Fermer le panneau de recherche

Appuyez sur Entrée pour rechercher ou ESC pour annuler.

1 Chroniques 10
Bible en Swahili de l’est


1 Basi Wafilisti wakapigana juu ya Israeli; nao watu wa Israeli wakakimbia mbele ya Wafilisti, wakaanguka wameuawa katika mlima Gilboa. 2 Nao Wafilisti wakamfuatia sana Sauli na wanawe; Wafilisti wakawaua Yonathani, na Abinadabu, na Malkishua, wana wa Sauli. 3 Tena vita vilikuwa vikali sana juu ya Sauli, na wapiga upinde wakampata; hata akafadhaika sana kwa sababu ya wapiga upinde. 4 Ndipo Sauli akamwambia yule mchukua silaha zake, Futa upanga wako, unichome nao, wasije watu hawa wasiotahiriwa wakanisimanga. Lakini huyo mchukua silaha zake akakataa; kwa sababu aliogopa sana. Basi Sauli akautwaa upanga wake, akauangukia. 5 Na mchukua silaha zake alipoona ya kuwa Sauli amekufa, yeye naye akauangukia upanga wake, akafa. 6 Hivyo Sauli akafa, na wanawe watatu; na nyumba yake yote wakafa pamoja. 7 Kisha watu wote wa Israeli, waliokuwa huko bondeni, walipoona ya kuwa wamekimbia, na ya kuwa Sauli na wanawe wamekufa, wakaiacha miji yao, wakakimbia; nao Wafilisti wakaenda wakakaa humo. 8 Hata ikawa siku ya pili yake Wafilisti walipokwenda kuwateka nyara hao waliouawa, walimwona Sauli na wanawe wameanguka juu ya mlima Gilboa. 9 Wakamvua mavazi, wakamtwalia kichwa, na silaha zake, kisha wakapeleka wajumbe kwenda nchi ya Wafilisti pande zote, ili kutangaza habari kwa sanamu zao, na kwa watu. 10 Wakaziweka silaha zake nyumbani mwa miungu yao, wakakikaza kichwa chake nyumbani mwa Dagoni. 11 Na watu wote wa Yabesh-gileadi waliposikia hayo yote Wafilisti waliyomtenda Sauli, 12 wakainuka mashujaa wote, wakautwaa mwili wake Sauli, na miili ya wanawe, wakaileta Yabeshi, wakaizika mifupa yao chini ya mwaloni huko Yabeshi, nao wakafunga muda wa siku saba. 13 Basi Sauli alikufa kwa sababu ya kosa lake alilomkosa Bwana, kwa sababu ya neno la Bwana, asilolishika; na tena kwa kutaka shauri kwa mwenye pepo wa utambuzi, aulize kwake, 14 asiulize kwa Bwana; kwa hiyo akamwua, na ufalme akamgeuzia Daudi, mwana wa Yese.

Cette Bible est dans le domaine public.