Un clic sur un verset envoie vers le comparateur de versions.
Proverbes 18.2 Bible en Swahili de l’est
1 Ajitengaye na wenzake hutafuta matakwa yake mwenyewe; Hushindana na kila shauri jema.2 Mpumbavu hapendezwi na ufahamu; Ila moyo wake udhihirike tu.3 Ajapo asiye haki, huja dharau pia; Na pamoja na aibu huja lawama. 4 Maneno ya kinywa cha mtu ni kama maji ya vilindi; Kijito kibubujikacho; chemchemi ya hekima. 5 Kukubali uso wake asiye haki si vizuri; Wala kumpotosha mwenye haki hukumuni. 6 Midomo ya mpumbavu huingia katika fitina, Na kinywa chake huita mapigo. 7 Kinywa cha mpumbavu ni uharibifu wake, Na midomo yake ni mtego wa nafsi yake. 8 Maneno ya mchongezi ni kama vitoweo; Nayo hushukia pande za ndani za tumbo. 9 Yeye naye aliye mvivu katika kazi yake, Ni ndugu yake aliye mharabu. 10 Jina la Bwana ni ngome imara; Mwenye haki huikimbilia, akawa salama. 11 Mali ya mtu tajiri ni mji wake wa nguvu; Ni kama ukuta mrefu katika mawazo yake. 12 Kabla ya uharibifu moyo wa mwanadamu hujivuna; Na kabla ya heshima hutangulia unyenyekevu. 13 Yeye ajibuye kabla hajasikia, Ni upumbavu na aibu kwake. 14 Roho ya mtu itastahimili udhaifu wake; Bali roho iliyovunjika nani awezaye kuistahimili? 15 Moyo wa mwenye busara hupata maarifa; Na sikio la mwenye hekima hutafuta maarifa. 16 Zawadi ya mtu humpatia nafasi; Humleta mbele ya watu wakuu. 17 Ajiteteaye kwanza huonekana kuwa ana haki; Lakini jirani yake huja na kumchunguza. 18 Kura hukomesha mashindano; Hukata maneno ya wakuu. 19 Ndugu aliyechukizwa ni mgumu kuliko mji wa nguvu; Na mashindano ni kama mapingo ya ngome. 20 Tumbo la mtu litajazwa matunda ya kinywa chake; Atashiba mazao ya midomo yake. 21 Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi; Na wao waupendao watakula matunda yake. 22 Apataye mke apata kitu chema; Naye ajipatia kibali kwa Bwana. 23 Maskini hutumia maombi; Bali tajiri hujibu kwa ukali. 24 Ajifanyiaye rafiki wengi ni kwa uangamivu wake mwenyewe; Lakini yuko rafiki aambatanaye na mtu kuliko ndugu.