Un clic sur un verset envoie vers le comparateur de versions.
Osée 6.1 Bible en Swahili de l’est
1 Njoni, tumrudie Bwana; maana yeye amerarua, na yeye atatuponya; yeye amepiga, na yeye atatufunga jeraha zetu. 2 Baada ya siku mbili atatufufua; siku ya tatu atatuinua, nasi tutaishi mbele zake. 3 Nasi na tujue, naam, tukaendelee kumjua Bwana; kutokea kwake ni yakini kama asubuhi; naye atatujilia kama mvua, kama mvua ya vuli iinyweshayo nchi. 4 Ee Efraimu, nikutendee nini? Ee Yuda, nikutendee nini? Kwa maana fadhili zenu ni kama wingu la asubuhi na kama umande utowekao mapema. 5 Kwa sababu hiyo nimewakata-kata kwa vinywa vya manabii; nimewaua kwa maneno ya kinywa changu; na hukumu yangu itatokea kama mwanga. 6 Maana nataka fadhili wala si sadaka; na kumjua Mungu kuliko sadaka za kuteketezwa. 7 Lakini wao wamelivunja hilo agano kama Adamu; huko wamenitenda mambo ya hiana. 8 Gileadi ni mji wa hao watendao maovu, umetiwa rangi ya damu. 9 Na kama vile makundi ya wanyang’anyi wamwoteavyo mtu, ndivyo kundi la makuhani wauavyo katika njia ielekeayo Shekemu; naam, wametenda mambo maovu sana. 10 Katika nyumba ya Israeli nimeona jambo bovu kabisa; huko uzinzi umeonekana katika Efraimu; Israeli ametiwa unajisi. 11 Tena, Ee Yuda, wewe umeandikiwa mavuno, hapo nitakapowarudisha wafungwa wa watu wangu.