Un clic sur un verset envoie vers le comparateur de versions.
1 Thessaloniciens 1.5 Bible en Swahili de l’est
Salutation et louange
1 Paulo, na Silwano, na Timotheo, kwa kanisa la Wathesalonike, lililo katika Mungu Baba, na katika Bwana Yesu Kristo. Neema na iwe kwenu na amani. 2 Twamshukuru Mungu siku zote kwa ajili yenu nyote, tukiwataja katika maombi yetu. 3 Wala hatuachi kuikumbuka kazi yenu ya imani, na taabu yenu ya upendo, na saburi yenu ya tumaini lililo katika Bwana wetu Yesu Kristo, mbele za Mungu Baba yetu. 4 Kwa maana, ndugu mnaopendwa na Mungu, twajua uteule wenu; 5 ya kwamba injili yetu haikuwafikia katika maneno tu, bali na katika nguvu, na katika Roho Mtakatifu, na uthibitifu mwingi; kama vile mnavyojua jinsi zilivyokuwa tabia zetu kwenu, kwa ajili yenu. 6 Nanyi mkawa wafuasi wetu na wa Bwana, mkiisha kulipokea neno katika dhiki nyingi, pamoja na furaha ya Roho Mtakatifu. 7 Hata mkawa kielelezo kwa watu wote waaminio katika Makedonia, na katika Akaya. 8 Maana kutoka kwenu neno la Mungu limevuma, si katika Makedonia na Akaya tu, ila na kila mahali imani yenu mliyo nayo kwa Mungu imeenea; hata hatuna haja sisi kunena lo lote. 9 Kwa kuwa wao wenyewe wanatangaza habari zetu, jinsi kulivyokuwa kuingia kwetu kwenu; na jinsi mlivyomgeukia Mungu mkaziacha sanamu, ili kumtumikia Mungu aliye hai, wa kweli; 10 na kumngojea Mwanawe kutoka mbinguni, ambaye alimfufua katika wafu, naye ni Yesu, mwenye kutuokoa na ghadhabu itakayokuja.