Un clic sur un verset envoie vers le comparateur de versions.
Zacharie 13.2 Bible en Swahili de l’est
1 Katika siku hiyo watu wa nyumba ya Daudi, na wenyeji wa Yerusalemu, watafunguliwa chemchemi kwa dhambi na kwa unajisi. 2 Kisha itakuwa katika siku hiyo, asema Bwana wa majeshi, nitakatilia mbali majina ya sanamu katika nchi, yasikumbukwe tena; pia nitawafukuza manabii, na roho ya uchafu, watoke katika nchi. 3 Tena itakuwa ya kwamba, mtu awaye yote atakapotoa unabii, basi baba yake na mama yake waliomzaa watamwambia, Hutaishi; kwa maana unanena maneno ya uongo kwa jina la Bwana; na baba yake na mama yake waliomzaa watamtumbua atoapo unabii. 4 Tena itakuwa siku hiyo, ya kwamba manabii, kila mmoja wao, atayaonea haya maono yake atoapo unabii; wala hawatavaa joho ya nywele ili kudanganya watu; 5 bali atasema, Mimi si nabii kamwe; mimi ni mkulima wa nchi; kwa maana nalifanywa mtumwa tokea ujana wangu. 6 Na mtu atamwambia, Je! Jeraha hizi ulizo nazo kati ya mikono yako ni nini? Naye atajibu, Ni jeraha nilizotiwa katika nyumba ya rafiki zangu. 7 Amka, Ee upanga, juu ya mchungaji wangu, na juu ya mtu aliye mwenzangu, asema Bwana wa majeshi; mpige mchungaji, nao kondoo watatawanyika; nami nitaugeuza mkono wangu juu ya wadogo. 8 Hata itakuwa, ya kwamba katika nchi yote mafungu mawili yatakatiliwa mbali, nao watakufa, asema Bwana; lakini fungu la tatu litabaki humo. 9 Nami nitalileta fungu lile la tatu na kulipitisha kati ya moto, nami nitawasafisha kama fedha isafishwavyo, nami nitawajaribu kama dhahabu ijaribiwavyo; wataliitia jina langu, nami nitawasikia; mimi nitasema, Watu hawa ndio wangu; nao watasema, Bwana ndiye Mungu wangu.