Un clic sur un verset envoie vers le comparateur de versions.
Psaumes 56.2 Bible en Swahili de l’est
Confiance dans la détresse
1 Mungu, unirehemu, maana yuko atakaye kunimeza, Mchana kutwa ananionea akileta vita. 2 Adui zangu wanataka kunimeza mchana kutwa, Maana waletao vita juu yangu kwa kiburi ni wengi. 3 Siku ya hofu yangu nitakutumaini Wewe; 4 Kwa msaada wa MUNGU nitalisifu neno lake. Nimemtumaini Mungu, sitaogopa; Mwenye mwili atanitenda nini? 5 Mchana kutwa wanapotosha maneno yangu, Mawazo yao yote ni juu yangu kunitakia mabaya. 6 Hukutanika, hujificha, huziangalia nyayo zangu, Kwa kuwa wameniotea nafsi yangu. 7 Je! Wataokoka kwa uovu wao? Ee Mungu, uwaangamize kwa hasira yako. 8 Umehesabu kutanga-tanga kwangu; Uyatie machozi yangu katika chupa yako; (Je! Hayamo katika kitabu chako?) 9 Ndipo adui zangu watarudi nyuma siku ile niitapo. Neno hili najua kuwa MUNGU yu upande wangu; 10 Kwa msaada wa MUNGU nitalisifu neno lake. Kwa msaada wa Bwana nitalisifu neno lake. 11 Nimemtumaini Mungu, sitaogopa; Mwanadamu atanitenda nini? 12 Ee Mungu, nadhiri zako zi juu yangu; Nitakutolea dhabihu za kushukuru. 13 Maana umeniponya nafsi yangu na mauti; Je! Hukuizuia miguu yangu isianguke? Ili nienende mbele za Mungu Katika nuru ya walio hai.