Un clic sur un verset envoie vers le comparateur de versions.
Esaïe 61.10 Bible en Swahili de l’est
Le salut proclamé
1 Roho ya Bwana MUNGU i juu yangu; kwa sababu Bwana amenitia mafuta niwahubiri wanyenyekevu habari njema; amenituma ili kuwaganga waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka uhuru wao, na hao waliofungwa habari za kufunguliwa kwao. 2 Kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa, na siku ya kisasi cha Mungu wetu; kuwafariji wote waliao; 3 kuwaagizia hao waliao katika Sayuni, wapewe taji ya maua badala ya majivu, mafuta ya furaha badala ya maombolezo, vazi la sifa badala ya roho nzito; wapate kuitwa miti ya haki, iliyopandwa na Bwana, ili atukuzwe. 4 Nao watajenga mahali pa kale palipoharibiwa, watapainua mahali palipokuwa ukiwa zamani, watatengeneza miji iliyoharibiwa, mahali palipoachwa kizazi baada ya kizazi. 5 Na wageni watasimama na kulisha makundi yenu, na watu wa kabila nyingine watakuwa wakulima wenu, na watunzaji wa mizabibu yenu. 6 Bali ninyi mtaitwa makuhani wa Bwana; watu watawaiteni wahudumu wa Mungu wetu; mtakula utajiri wa mataifa, na kujisifia utukufu wao. 7 Badala ya aibu yenu mtapata maradufu, na badala ya fedheha wataifurahia sehemu yao; basi katika nchi yao watamiliki maradufu; furaha yao itakuwa ya milele. 8 Maana mimi, Bwana, naipenda hukumu ya haki, nauchukia wivi na uovu; nami nitawalipa malipo katika kweli, nitaagana nao agano la milele. 9 Na kizazi chao kitajulikana katika mataifa, na uzao wao katika kabila za watu; wote wawaonao watakiri ya kuwa wao ni kizazi kilichobarikiwa na Bwana. 10 Nitafurahi sana katika Bwana, nafsi yangu itashangilia katika Mungu wangu; maana amenivika mavazi ya wokovu, amenifunika vazi la haki, kama bwana arusi ajipambavyo kwa kilemba cha maua, na kama bibi arusi ajipambavyo kwa vyombo vya dhahabu. 11 Maana kama nchi itoavyo machipuko yake, na kama bustani ioteshavyo vitu vilivyopandwa ndani yake; ndivyo Bwana MUNGU atakavyootesha haki na sifa mbele ya mataifa yote.