Un clic sur un verset envoie vers le comparateur de versions.
Josué 1.10 Bible en Swahili de l’est
1 Ikawa baada ya kufa kwake Musa, mtumishi wa Bwana, Bwana akamwambia Yoshua, mwana wa Nuni, mtumishi wa Musa, akasema, 2 Musa mtumishi wangu amekufa; haya basi, ondoka, vuka mto huu wa Yordani; wewe na watu hawa wote, mkaende hata nchi niwapayo wana wa Israeli. 3 Kila mahali zitakapopakanyaga nyayo za miguu yenu, nimewapa ninyi, kama nilivyomwapia Musa. 4 Tangu jangwa hili na mlima huu, Lebanoni, mpaka mto ule mkubwa, mto wa Frati, nchi yote ya Wahiti, tena mpaka bahari ile kubwa upande wa machweo ya jua, hapo ndipo patakapokuwa mpaka wenu. 5 Hapatakuwa mtu ye yote atakayeweza kusimama mbele yako siku zote za maisha yako; kama nilivyokuwa pamoja na Musa, ndivyo nitakavyokuwa pamoja na wewe; sitakupungukia wala sitakuacha. 6 Uwe hodari na moyo wa ushujaa, maana ni wewe utakayewarithisha watu hawa nchi hii niliyowaapia baba zao ya kwamba nitawapa. 7 Uwe hodari tu na ushujaa mwingi, uangalie kutenda sawasawa na sheria yote aliyokuamuru Musa mtumishi wangu; usiiache, kwenda mkono wa kuume, au wa kushoto, upate kufanikiwa sana kila uendako. 8 Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana. 9 Je! Si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na moyo wa ushujaa; usiogope wala usifadhaike; kwa kuwa Bwana, Mungu wako, yu pamoja nawe kila uendako.10 Ndipo Yoshua akawaamuru maakida wa watu, akisema,11 Piteni katikati ya matuo, mkawaamuru hao watu, mkisema, Fanyeni tayari vyakula; kwa maana baada ya siku tatu mtavuka mto huu wa Yordani, ili kuingia na kuimiliki nchi awapayo Bwana, Mungu wenu, mpate kuimiliki. 12 Tena Yoshua akawaambia Wareubeni, na Wagadi, na hao wa nusu ya kabila ya Manase, akasema, 13 Likumbukeni neno lile alilowaamuru Musa mtumishi wa Bwana, akisema, Bwana, Mungu wenu, anawapa ninyi raha, naye atawapa nchi hii. 14 Wake zenu, na watoto wenu, na makundi yenu, watakaa katika nchi aliyowapa Musa ng’ambo ya Yordani; bali ninyi mtavuka mbele ya ndugu zenu, hali mmevikwa silaha zenu, watu wote wenye nguvu, na ushujaa, ili mpate kuwasaidia; 15 hata Bwana atakapowapa ndugu zenu raha, kama alivyowapa ninyi, na wao pia wamepata kuimiliki nchi awapayo Bwana, Mungu wenu; ndipo mtakapoirudia nchi ya milki yenu na kuimiliki, ambayo Musa mtumishi wa Bwana aliwapeni ng’ambo ya Yordani upande wa maawio ya jua. 16 Wakamjibu Yoshua, wakasema, Hayo yote uliyotuamuru tutayafanya, na kila mahali utakakotutuma tutakwenda. 17 Kama vile tulivyomsikiliza Musa katika mambo yote, ndivyo tutakavyokusikiliza wewe; Bwana, Mungu wako, na awe pamoja nawe tu, kama alivyokuwa pamoja na Musa. 18 Kila mtu atakayeiasi amri yako, asiyasikilize maneno yako katika mambo yote utakayomwamuru, atauawa. Uwe hodari na moyo wa ushujaa, hilo tu.