Un clic sur un verset envoie vers le comparateur de versions.
Psaumes 141.3 Bible en Swahili de l’est
1 Ee Bwana, nimekuita, unijie hima, Uisikie sauti yangu nikuitapo. 2 Sala yangu ipae mbele zako kama uvumba, Kuinuliwa mikono yangu kama dhabihu ya jioni.3 Ee Bwana, uweke mlinzi kinywani pangu, Mngojezi mlangoni pa midomo yangu.4 Usiuelekeze moyo wangu kunako jambo baya, Nisiyazoelee matendo yasiyofaa, Pamoja na watu watendao maovu; Wala nisile vyakula vyao vya anasa. 5 Mwenye haki na anipige, itakuwa fadhili; Anikemee, itakuwa kama mafuta kichwani; Kichwa changu kisikatae, Maana siachi kusali kati ya mabaya yao. 6 Makadhi wao wakiangushwa kando ya genge, Watayasikia maneno yangu, maana ni matamu. 7 Kama kupasua kuni na kuzichanja juu ya nchi, Ndivyo ilivyo mifupa yetu mdomoni pa kuzimu. 8 Macho yangu yanakuelekea Wewe, MUNGU Bwana, Nimekukimbilia Wewe, usiniache nafsi yangu. 9 Unilinde na mtego walionitegea, Na matanzi yao watendao maovu. 10 Wabaya na waanguke katika nyavu zao wenyewe, Pindi mimi ninapopita salama.