Fermer le panneau de recherche

Appuyez sur Entrée pour rechercher ou ESC pour annuler.

Néhémie 5.6
Bible en Swahili de l’est


Attitude désintéressée de Néhémie

1 Ndipo kukatokea kilio kikuu cha watu, na wake zao, juu ya ndugu zao Wayahudi.
2 Maana, walikuwako watu waliosema, Sisi, na wana wetu na binti zetu, tu wengi; na tupate ngano, tule, tukaishi.
3 Tena walikuwako wengine waliosema, Tumeweka rehani mashamba yetu, na mizabibu yetu, na nyumba zetu; tupate ngano, kwa sababu ya njaa.
4 Tena walikuwako wengine waliosema, Tumekopa fedha ili kulipa kodi ya mfalme kwa kuweka rehani mashamba yetu, na mizabibu yetu.
5 Walakini miili yetu ni kama miili ya ndugu zetu, na watoto wetu kama watoto wao; kumbe! Mnawatia utumwani wana wetu na binti zetu kuwa watumishi, na baadhi ya binti zetu wamekwisha kutiwa utumwani; wala hatuwezi kujiepusha na hayo; maana watu wengine wana mashamba yetu na mizabibu yetu.
6 Nami nilikasirika sana, niliposikia kilio chao, na maneno hayo.
7 Ndipo nikafanya shauri na nafsi yangu, nikagombana na wakuu na mashehe, nikawaambia, Mnatoza watu riba, kila mtu ndugu yake. Nikakutanisha mkutano mkubwa ili kushindana nao.
8 Nikawaambia, Sisi kwa kadiri ya uwezo wetu tumewakomboa ndugu zetu Wayahudi, waliouzwa kwa makafiri; na ninyi mnataka kuwauza ndugu zenu, tena kuwauza ili sisi tuwanunue? Wakanyamaza kimya, wasiweze kusema neno lo lote.
9 Tena nalisema, Neno hili mnalolitenda si jema; je! Haiwapasi ninyi kwenda katika kicho cha Mungu wetu, kwa sababu ya mashutumu ya makafiri adui zetu?
10 Na mimi pia, na ndugu zangu, na watumishi wangu, twawakopesha fedha na ngano ili kupata faida? Tafadhali na tuliache jambo hili la riba.
11 Naomba, warudishieni leo hivi mashamba yao, na mashamba yao ya mizabibu, na mashamba yao ya mizeituni, na nyumba zao, na lile fungu la mia la fedha, na la ngano, na la divai, na la mafuta, mnalowatoza.
12 Ndipo wakasema, Tutawarudishia, wala hatutataka kitu kwao; tutafanya hivyo, kama ulivyosema. Kisha nikawaita makuhani, nikawaapisha, ya kwamba watafanya kama ahadi hiyo.
13 Tena nikakung’uta nguo yangu, nikasema, Mungu na amkung’ute vivyo hivyo kila mtu nyumbani mwake, na kazini mwake, asiyeitimiza ahadi hiyo; naam, na akung’utwe vivyo hivyo, na kuwa hana kitu. Mkutano wote wakasema, Amina; wakamhimidi Bwana. Nao watu wakafanya kama ahadi hiyo.
14 Tena tangu wakati huo nilipowekwa kuwa liwali wao katika nchi ya Yuda, tangu mwaka wa ishirini hata mwaka wa thelathini na mbili wa Artashasta mfalme, yaani, miaka kumi na miwili, mimi na ndugu zangu hatukula chakula cha liwali.
15 Lakini maliwali wa kwanza walionitangulia, wakawalemea watu, wakawatwalia chakula na mvinyo, zaidi ya shekeli arobaini za fedha; tena watumwa wao nao wakatawala juu ya watu; lakini mimi sikufanya hivyo, kwa kuwa nalimcha Mungu.
16 Naam, hata kazi ya ukuta huu tena nikaishika sana, wala hatukununua mashamba; na watumishi wangu wote wakakusanyika huko kazini.
17 Pamoja na hayo wakawako mezani pangu, katika Wayahudi na mashehe, watu mia na hamsini, zaidi ya wale waliotujia kutoka kwa makafiri waliotuzunguka.
18 Basi, maandalio yaliyoandaliwa kwa siku moja yalikuwa ng’ombe mmoja, na kondoo wazuri sita; tena nikaandaliwa kuku, na mara moja katika siku kumi akiba ya mvinyo ya namna zote; wala kwa hayo yote sikukidai chakula cha liwali, kwa kuwa utumwa ulikuwa mzito juu ya watu hao.
19 Unikumbukie, Ee Mungu wangu, kwa mema, yote niliyowafanyia watu hawa.

Cette Bible est dans le domaine public.