Un clic sur un verset envoie vers le comparateur de versions.
Jean 21 Bible en Swahili de l’est
La pêche miraculeuse
Voir Jean 21.1 en vidéo
1 Baada ya hayo Yesu alijidhihirisha tena kwa wanafunzi wake, penye bahari ya Tiberia, naye alijidhihirisha hivi. 2 Simoni Petro, na Tomaso aitwaye Pacha, na Nathanaeli wa Kana ya Galilaya, na wana wa Zebedayo, na wengine wawili wa wanafunzi wake, walikuwapo pamoja. 3 Simoni Petro aliwaambia, Naenda kuvua samaki. Nao wakamwambia, Sisi nasi tutakwenda nawe. Basi wakaondoka, wakapanda chomboni; ila usiku ule hawakupata kitu. 4 Hata asubuhi kulipokucha, Yesu alisimama ufuoni; walakini wanafunzi hawakujua ya kuwa ni Yesu. 5 Basi Yesu akawaambia, Wanangu, mna kitoweo? Wakamjibu, La. 6 Akawaambia, Litupeni jarife upande wa kuume wa chombo, nanyi mtapata. Basi wakatupa; wala sasa hawakuweza kulivuta tena kwa sababu ya wingi wa samaki. 7 Basi yule mwanafunzi ambaye Yesu alimpenda akamwambia Petro, Ndiye Bwana. Naye Simoni Petro, aliposikia ya kwamba ni Bwana, akajifunga vazi lake, (maana alikuwa uchi), akajitupa baharini. 8 Na hao wanafunzi wengine wakaja katika mashua; maana hawakuwa mbali na nchi kavu; ila yapata dhiraa mia mbili; huku wakilikokota lile jarife lenye samaki. 9 Basi waliposhuka pwani, wakaona huko moto wa makaa, na juu yake pametiwa samaki, na mkate. 10 Yesu akawaambia, Leteni hapa baadhi ya samaki mliowavua sasa hivi. 11 Basi Simoni Petro akapanda chomboni, akalivuta jarife pwani, limejaa samaki wakubwa, mia hamsini na watatu; na ijapokuwa ni wengi namna hiyo, jarife halikupasuka. 12 Yesu akawaambia, Njoni mfungue kinywa. Wala hakuna mtu katika wale wanafunzi aliyethubutu kumwuliza, U nani wewe? Wakijua ya kuwa ni Bwana. 13 Yesu akaenda akautwaa mkate, akawapa, na samaki vivyo hivyo. 14 Hiyo ndiyo mara ya tatu ya Yesu kuonekana na wanafunzi wake baada ya kufufuka katika wafu.
Voir Jean 21.15 en vidéo
15 Basi walipokwisha kula, Yesu akamwambia Simoni Petro, Je! Simoni wa Yohana, wewe wanipenda kuliko hawa? Akamwambia , Naam ,Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, Lisha wana-kondoo wangu. 16 Akamwambia tena mara ya pili, Simoni wa Yohana, wanipenda? Akamwambia, Ndiyo, Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, Chunga kondoo zangu. 17 Akamwambia mara ya tatu, Simoni wa Yohana, wanipenda? Petro alihuzunika kwa vile alivyomwambia mara ya tatu, Wanipenda? Akamwambia, Bwana, wewe wajua yote; wewe umetambua ya kuwa nakupenda. Yesu akamwambia, Lisha kondoo zangu. 18 Akasema, Amin, amin, nakuambia, Wakati ulipokuwa kijana, ulikuwa ukijifunga mwenyewe na kwenda utakako; lakini utakapokuwa mzee, utainyosha mikono yako, na mwingine atakufunga na kukuchukua usikotaka. 19 Akasema neno hilo kwa kuonyesha ni kwa mauti gani atakayomtukuza Mungu. Naye akiisha kusema hayo akamwambia, Nifuate. 20 Petro akageuka akamwona yule mwanafunzi aliyependwa na Yesu anafuata; (ndiye huyo aliyeegama kifuani pake wakati wa kula chakula cha jioni, akasema, Bwana, ni nani akusalitiye?) 21 Basi Petro akamwona huyo, akamwambia Yesu, Bwana, na huyu je? 22 Yesu akamwambia, Ikiwa nataka huyu akae hata nijapo, imekupasaje wewe? Wewe unifuate mimi. 23 Basi neno hilo lilienea katikati ya ndugu ya kwamba mwanafunzi yule hafi. Walakini Yesu hakumwambia ya kwamba hafi; bali, Ikiwa nataka huyu akae hata nijapo, imekupasaje wewe? 24 Huyu ndiye yule mwanafunzi ayashuhudiaye haya, na aliyeyaandika haya: nasi twajua ya kuwa ushuhuda wake ni kweli. 25 Kuna na mambo mengi aliyoyafanya Yesu; ambayo yakiandikwa moja moja, nadhani hata ulimwengu usingetosha kwa vile vitabu vitakavyoandikwa.