Un clic sur un verset envoie vers le comparateur de versions.
Esther 5.14 Bible en Swahili de l’est
1 Ikawa siku ya tatu Esta alijivika mavazi yake ya kifalme, akasimama katika ua wa ndani wa nyumba ya mfalme, kuielekea nyumba ya mfalme; naye mfalme akaketi juu ya kiti chake cha enzi katika nyumba ya mfalme, kuuelekea mlango wa nyumba. 2 Ikawa, mfalme alipomwona malkia Esta amesimama uani, yeye akapata kibali machoni pake; naye mfalme akamnyoshea Esta fimbo ya dhahabu aliyokuwa nayo mkononi. Basi Esta akakaribia, akaigusa ncha ya fimbo. 3 Mfalme akamwambia, Malkia Esta, wataka nini? Nayo ni haja gani uliyo nayo? Utapewa hata nusu ya ufalme. 4 Esta akasema, Mfalme akiona vema, na aje leo, mfalme na Hamani, kwenye karamu niliyomwandalia. 5 Basi mfalme akasema, Mhimize Hamani, ili ifanyike kama Esta alivyosema. Hivyo mfalme na Hamani wakafika katika karamu ile aliyoiandaa Esta. 6 Basi mfalme akamwambia Esta pale penye karamu ya divai, Dua yako ni nini? Nawe utapewa; na haja yako ni nini? Hata nusu ya ufalme utafanyiziwa. 7 Esta akajibu, na kusema, Dua yangu ni hii, na haja yangu ni hii, 8 Ikiwa nimepata kibali machoni pa mfalme, na mfalme akiona vema kunipa niombalo, na kunifanyizia haja yangu, na aje tena mfalme na Hamani kwenye karamu nitakayowaandalia, nami kesho nitafanya kama vile mfalme alivyosema. 9 Basi Hamani alitoka siku ile kwa furaha na ukunjufu wa moyo; lakini Hamani alipomwona Mordekai mlangoni pa mfalme, ya kwamba hasimami wala kutetemeka mbele yake, alijaa ghadhabu juu ya Mordekai. 10 Walakini Hamani akajizuia, akaenda zake nyumbani kwake; akatuma kuwaita rafiki zake na Zereshi mkewe. 11 Naye Hamani akawasimulia habari za fahari ya mali zake, na wingi wa watoto wake, nayo mambo yote pia ambayo mfalme amemfanikisha katika hayo, na jinsi alivyompandisha juu ya maakida na watumishi wa mfalme. 12 Zaidi ya hayo Hamani akasema, Naye malkia Esta hakumkaribisha mtu ye yote pamoja na mfalme katika karamu aliyoiandaa, ila mimi peke yangu; hata na kesho pia nimealikwa naye pamoja na mfalme. 13 Bali haya yote yanifaa nini, pindi nimwonapo yule Mordekai, Myahudi, ameketi mlangoni pa mfalme?14 Basi Zereshi mkewe akamwambia, na rafiki zake wote, Na ufanyizwe mti wa mikono hamsini urefu wake, na kesho asubuhi useme na mfalme ili Mordekai atundikwe juu yake; ndipo utakapoingia kwa kicheko pamoja na mfalme karamuni. Basi neno likampendeza Hamani, akaufanyiza ule mti.