Un clic sur un verset envoie vers le comparateur de versions.
Esaïe 62.3 Bible en Swahili de l’est
1 Kwa ajili ya Sayuni sitanyamaza, na kwa ajili ya Yerusalemu sitatulia, hata haki yake itakapotokea kama mwangaza, na wokovu wake kama taa iwakayo. 2 Na mataifa wataiona haki yako, na wafalme wote watauona utukufu wako; nawe utaitwa jina jipya, litakalotajwa na kinywa cha Bwana.3 Nawe utakuwa taji ya uzuri katika mkono wa Bwana, na kilemba cha kifalme mkononi mwa Mungu wako.4 Hutaitwa tena Aliyeachwa, wala nchi yako haitaitwa tena, Ukiwa; bali utaitwa Hefsiba; na nchi yako Beula;kwa kuwa Bwana anakufurahia ,na nchi yako itaolewa. 5 Maana kama vile kijana amwoavyo mwanamwali, ndivyo wana wako watakavyokuoa wewe; na kama vile bwana arusi amfurahiavyo bibi arusi, ndivyo Mungu wako atakavyokufurahia wewe. 6 Nimeweka walinzi juu ya kuta zako, Ee Yerusalemu; hawatanyamaza mchana wala usiku; ninyi wenye kumkumbusha Bwana, msiwe na kimya; 7 wala msimwache akae kimya, mpaka atakapoufanya imara Yerusalemu, na kuufanya kuwa sifa duniani. 8 Bwana ameapa kwa mkono wake wa kuume, na kwa mkono wa nguvu zake, Hakika sitawapa adui zako nafaka yako tena kuwa chakula chao; wala wageni hawatakunywa divai yako, uliyoifanyia kazi. 9 Lakini walioivuna, ndio watakaoila, na kumhimidi Bwana; na walioichuma, ndio watakaoinywa, ndani ya nyua za patakatifu pangu. 10 Piteni, piteni, katika malango; Itengenezeni njia ya watu; Tutieni, tutieni barabara; toeni mawe yake; Twekeni bendera kwa ajili ya kabila za watu. 11 Tazama, Bwana ametangaza habari mpaka mwisho wa dunia, Mwambieni binti Sayuni, Tazama, wokovu wako unakuja; Tazama, thawabu yake i pamoja naye, Na malipo yake yako mbele zake. 12 Nao watawaita, Watu watakatifu, Waliokombolewa na Bwana; Nawe utaitwa, Aliyetafutwa, Mji usioachwa.