Un clic sur un verset envoie vers le comparateur de versions.
Job 3 Bible en Swahili de l’est
Dialogue entre Job et ses amis
Intervention n° 1 de Job
1 Baada ya hayo Ayubu akafunua kinywa chake, na kuilaani siku yake. 2 Ayubu akajibu, na kusema; 3 Na ipotelee mbali ile siku niliyozaliwa mimi, Na ule usiku uliosema, Mtoto mume ametungishwa mimba. 4 Siku hiyo na iwe giza; Mungu asiiangalie toka juu, Wala mwanga usiiangazie. 5 Ishikwe na giza, giza tupu, kuwa yake; Wingu na likae juu yake; Chote kiifanyacho siku kuwa giza na kiitishe. 6 Tena usiku huo, na ushikwe na giza kuu; Usihesabiwe katika siku za mwaka; Wala kutiwa katika hesabu ya miezi. 7 Tazama, usiku huo na uwe tasa; Wala isiwe ndani yake sauti ya shangwe. 8 Na waulaani hao waulaanio mchana, Hao walio tayari kumwamsha huyo lewiathani. 9 Nyota za mapambazuko yake na ziwe giza; Na utafute mwanga lakini usiupate; Wala usiyaone makope ya asubuhi; 10 Kwa sababu haukuifunga milango ya tumbo la mamangu. Wala kunifichia taabu machoni. 11 Mbona si kufa mimi tokea mimbani? Mbona nisitoe roho hapo nilipotoka tumboni? 12 Mbona hayo magoti kunipokea? Au hayo maziwa, hata nikanyonya? 13 Maana hapo ningelala na kutulia; Ningelala usingizi; na kupata kupumzika; 14 Pamoja na wafalme na washauri wa dunia, Hao waliojijengea maganjoni; 15 Au pamoja na wakuu wenye dhahabu, Waliozijaza fedha nyumba zao; 16 Au, kama kuzikwa mimba iliyoharibika, nisingekuwako; Kama wachanga wasiouona mwanga kabisa. 17 Huko waovu huacha kusumbua; Huko nako hao waliochoka wapumzika 18 Huko wafungwa waona raha pamoja; Hawaisikii sauti yake msimamizi. 19 Wakuu na wadogo wako huko; Mtumishi yu huru kwa bwana wake. 20 Mbona yeye aliye mashakani kupewa mwanga, Na hao wenye uchungu rohoni kupewa uhai; 21 Ambao wangojea mauti, lakini hawayapati; Na kuyachimbulia zaidi ya kutafuta hazina iliyostirika; 22 Ambao wafurahi mno, Na kushangilia watakapoliona kaburi? 23 Kwa nini mtu aliyezibiwa njia kupewa mwanga, Ambaye Mungu amemzingira kwa ukingo? 24 Kwani kuugua kwangu kwaja kana kwamba ni chakula, Na kunguruma kwangu kumemiminika kama maji. 25 Maana jambo hilo nichalo hunipata, Nalo linitialo hofu hunijilia. 26 Mimi sioni raha, wala situlii, wala kupumzika; Lakini huja taabu.