Fermer le panneau de recherche

Appuyez sur Entrée pour rechercher ou ESC pour annuler.

Psaumes 38.18
Bible en Swahili de l’est


1 Ee Bwana, usinilaumu katika ghadhabu yako, Wala usiniadhibu kwa ukali wa hasira yako. 2 Kwa maana mishale yako imenichoma, Na mkono wako umenipata. 3 Hamna uzima katika mwili wangu Kwa sababu ya ghadhabu yako. Wala hamna amani mifupani mwangu Kwa sababu ya hatia zangu. 4 Maana dhambi zangu zimenifunikiza kichwa, Kama mzigo mzito zimenilemea mno. 5 Jeraha zangu zinanuka, zimeoza, Kwa sababu ya upumbavu wangu. 6 Nimepindika na kuinama sana, Mchana kutwa nimekwenda nikihuzunika. 7 Maana viuno vyangu vimejaa homa, Wala hamna uzima katika mwili wangu. 8 Nimedhoofika na kuchubuka sana, Nimeugua kwa fadhaa ya moyo wangu. 9 Bwana, haja zangu zote ziko mbele zako, Kuugua kwangu hakukusitirika kwako. 10 Moyo wangu unapwita-pwita, Nguvu zangu zimeniacha; Nuru ya macho yangu nayo imeniondoka. 11 Wanipendao na rafiki zangu wanasimama mbali na pigo langu; Naam, karibu zangu wamesimama mbali. 12 Nao wanaoutafuta uhai wangu hutega mitego; Nao wanaotaka kunidhuru hunena mabaya; Na kufikiri hila mchana kutwa. 13 Lakini kama kiziwi sisikii, Nami ni kama bubu asiyefumbua kinywa chake. 14 Naam, nimekuwa kama mtu asiyesikia, Ambaye hamna hoja kinywani mwake. 15 Kwa kuwa nakungoja Wewe, Bwana, Wewe utajibu, Ee Bwana, Mungu wangu. 16 Maana nalisema, Wasije wakanifurahia; Mguu wangu ukiteleza wajitukuza juu yangu. 17 Kwa maana mimi ni karibu na kusita, Na maumivu yangu yako mbele yangu daima. 18 Kwa maana nitaungama uovu wangu, Na kusikitika kwa dhambi zangu. 19 Lakini adui zangu ni wazima wenye nguvu, Nao wanaonichukia bure wamekuwa wengi. 20 Naam, wakilipa mabaya kwa mema, Huwa adui zangu kwa kuwa nalifuata lililo jema. 21 Wewe, Bwana, usiniache, Mungu wangu, usijitenge nami. 22 Ufanye haraka kunisaidia, Ee Bwana, wokovu wangu.

Cette Bible est dans le domaine public.