Un clic sur un verset envoie vers le comparateur de versions.
Cantique 5.12 Bible en Swahili de l’est
1 Naingia bustanini mwangu, umbu langu, bibi arusi, Nachuma manemane yangu na rihani, Nala sega la asali na asali yangu, Nanywa divai yangu na maziwa. Kaleni, rafiki zangu, kanyweni, Naam, nyweni sana, wapendwa wangu. 2 Nalikuwa nimelala, lakini moyo wangu u macho, Sikiliza! Mpendwa wangu anabisha! Nifungulie, umbu langu, mpenzi wangu, Hua wangu, mkamilifu wangu, Kwa maana kichwa changu kimelowa umande, Nywele zangu zina manyunyu ya usiku. 3 Nimeivua kanzu yangu; niivaeje? Nimeitawadha miguu; niichafueje? 4 Mpendwa wangu aliutia mkono wake tunduni, Na moyo wangu ukachomeka kwa ajili yake. 5 Nikaondoka nimfungulie mpendwa wangu; Mikono yangu ilidondoza manemane, Na vidole vyangu matone ya manemane, Penye vipini vya komeo. 6 Nalimfungulia mpendwa wangu, Lakini mpendwa wangu amegeuka amepita; (Nimezimia nafsi yangu aliponena), Nikamtafuta, nisimpate, Nikamwita, asiniitikie. 7 Walinzi wazungukao mjini waliniona, Wakanipiga na kunitia jeraha, Walinzi walindao kuta zake Wakaninyang’anya shela yangu. 8 Nawasihi, enyi binti za Yerusalemu, Ninyi mkimwona mpendwa wangu, Ni nini mtakayomwambia? Ya kwamba nazimia kwa mapenzi. 9 Mpendwa wa namna gani ni mpendwa wako, Wewe uliye mzuri katika wanawake, Mpendwa wa namna gani ni mpendwa wako, Hata wewe utusihi hivyo? 10 Mpendwa wangu ni mweupe, tena mwekundu, Mashuhuri miongoni mwa elfu kumi; 11 Kichwa chake ni kama dhahabu safi sana, Nywele zake ni za ukoka, nyeusi kama kunguru;12 Macho yake ni kama hua penye vijito, Wakioga kwa maziwa, wakiikalia mito iliyojaa;13 Mashavu yake ni kama matuta ya rihani, Ambayo hufanyizwa manukato; Midomo yake ni kama nyinyoro, Inadondoza matone ya manemane; 14 Mikono yake ni kama mianzi ya dhahabu, lliyopambwa kwa zabarajadi; Kiwiliwili chake kama kazi ya pembe, Iliyonakishiwa kwa yakuti samawi; 15 Miguu yake ni kama nguzo za marimari, Zilizowekwa juu ya misingi ya dhahabu; Sura yake ni kama Lebanoni, Ni bora mfano wa mierezi; 16 Kinywa chake kimejaa maneno matamu, Ndiye mzuri sana pia pia. Ni huyu mpendwa wangu, ni huyu rafiki yangu, Enyi binti za Yerusalemu.