Un clic sur un verset envoie vers le comparateur de versions.
Genèse 12 Bible en Swahili de l’est
1 Bwana akamwambia Abramu, Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha; 2 nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako; nawe uwe baraka; 3 nami nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa. 4 Basi Abramu akaenda, kama Bwana alivyomwamuru; Lutu akaenda pamoja naye. Naye Abramu alikuwa mtu wa miaka sabini na mitano alipotoka Harani. 5 Abramu akamchukua Sarai mkewe, na Lutu mwana wa nduguye, na vitu vyao vyote walivyokuwa wamejipatia na hao watu waliowapata huko Harani, wakatoka ili kwenda nchi ya Kanaani; nao wakaingia katika nchi ya Kanaani. 6 Abramu akapita katikati ya nchi mpaka mahali patakatifu pa Shekemu; mpaka mwaloni wa More. Na Wakanaani siku zile walikaa katika nchi hiyo. 7 Bwana akamtokea Abramu, akasema, Uzao wako nitawapa nchi hii. Naye huko akamjengea madhabahu Bwana aliyemtokea. 8 Kisha akaondoka huko akaenda mpaka mlima ulio upande wa mashariki wa Betheli, akaipiga hema yake; alikuwa na Betheli upande wa magharibi, na Ai upande wa mashariki, akamjengea Bwana madhabahu huko, akaliitia jina la Bwana. 9 Naye Abramu akasafiri, akazidi kwenda pande za kusini. 10 Basi kulikuwa njaa katika nchi ile; Abramu akashuka Misri, akae huko kwa muda maana njaa ilikuwa nzito katika nchi. 11 Ikawa alipokuwa karibu kuingia Misri, akamwambia Sarai mkewe, Tazama, najua ya kuwa u mwanamke mzuri wa uso; 12 basi itakuwa, Wamisri watakapokuona watasema, Huyu ni mkewe; kisha wataniua mimi na wewe watakuacha hai. 13 Tafadhali useme, wewe u ndugu yangu, iwe heri kwangu kwa ajili yako, na nafsi yangu iishi kwa ajili yako. 14 Basi ikawa Abramu alipofika Misri, Wamisri wakamwona huyo mwanamke ya kwamba yeye ni mzuri sana. 15 Wakuu wa Farao wakamwona, nao wakamsifu kwa Farao; basi yule mwanamke akachukuliwa nyumbani mwa Farao. 16 Naye akamtendea Abramu mema kwa ajili yake; naye alikuwa na kondoo na ng’ombe, na punda waume, na watumwa, na wajakazi, na punda wake, na ngamia. 17 Lakini Bwana akampiga Farao na nyumba yake mapigo makuu, kwa ajili ya Sarai, mkewe Abramu. 18 Ndipo Farao akamwita Abramu, akasema, N’nini hili ulilonitendea? Mbona hukuniambia ya kuwa huyo ni mkeo? 19 Mbona ulisema, Huyo ni umbu langu, hata nikamtwaa kuwa mke wangu? Basi sasa, huyo mke wako umchukue, uende zako. 20 Farao akawaagiza watu kwa ajili yake, wakampeleka njiani, na mkewe, na kila alichokuwa nacho.