Un clic sur un verset envoie vers le comparateur de versions.
Proverbes 14.12 Bible en Swahili de l’est
1 Kila mwanamke aliye na hekima hujenga nyumba yake; Bali aliye mpumbavu huibomoa kwa mikono yake mwenyewe. 2 Yeye aendaye kwa unyofu wake humcha Bwana; Bali aliye mkaidi katika njia zake humdharau. 3 Katika kinywa cha mpumbavu mna fimbo ya kiburi, Bali midomo ya wenye hekima huwahifadhi. 4 Zizi ni safi ambapo hapana ng’ombe; Bali nguvu za ng’ombe zaleta faida nyingi. 5 Shahidi mwaminifu hatasema uongo; Bali shahidi wa uongo, pumzi zake ni uongo. 6 Mwenye dharau hutafuta hekima, asiipate; Bali maarifa huwa mepesi kwa mwenye ufahamu. 7 Toka mbele ya uso wa mpumbavu, Maana hutaona kwake midomo ya maarifa. 8 Akili za mwenye busara ni kujua njia yake; Lakini upumbavu wa wapumbavu ni udanganyifu. 9 Wapumbavu huidharau hatia; Bali upo upendeleo kwa wenye haki. 10 Moyo huujua uchungu wa nafsi yake, Wala mgeni haishiriki furaha yake. 11 Nyumba ya mtu mbaya itabomolewa; Bali hema ya mwenye haki itafanikiwa.12 Iko njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu, Lakini mwisho wake ni njia za mauti.13 Hata wakati wa kucheka moyo huwa na huzuni; Na mwisho wa furaha ni uzito wa moyo. 14 Ageukaye moyoni hushiba njia zake mwenyewe; Na mtu mwema ataridhika nafsini mwake. 15 Mjinga huamini kila neno; Bali mwenye busara huangalia sana aendavyo. 16 Mwenye hekima huogopa, akajitenga na uovu; Bali mpumbavu ana ufidhuli, na kujitumai. 17 Yeye aonaye hasira upesi atatenda kwa ujinga; Na mtu mwenye hila mbaya huzirwa. 18 Wajinga hurithi upumbavu; Bali wenye busara huvikwa taji ya maarifa. 19 Wabaya huinama mbele ya wema, Na wasio haki malangoni mwao wenye haki. 20 Maskini huchukiwa hata na jirani yake; Bali tajiri ana rafiki wengi. 21 Amdharauye mwenzake afanya dhambi; Bali amhurumiaye maskini ana heri. 22 Je! Hawakosi wawazao mabaya? Bali fadhili na kweli zina wao wawazao mema. 23 Katika kila kazi mna faida; Bali maneno ya midomo huleta hasara tu. 24 Taji ya wenye hekima ni mali zao; Bali upumbavu wa wajinga ni upumbavu tu. 25 Shahidi wa kweli huponya nafsi za watu; Bali atoaye uongo hudanganya. 26 Kumcha Bwana ni tumaini imara; Watoto wake watakuwa na kimbilio. 27 Kumcha Bwana ni chemchemi ya uzima, Ili kuepukana na tanzi za mauti. 28 Utukufu wa mfalme ni wingi wa watu wake; Bali uchache wa watu ni uharibifu wa mkuu wao. 29 Asiye mwepesi wa hasira ana fahamu nyingi; Bali mwenye roho ya hamaki hutukuza upumbavu. 30 Moyo ulio mzima ni uhai wa mwili; Bali husuda ni ubovu wa mifupa. 31 Amwoneaye maskini humsuta Muumba wake; Bali yeye awahurumiaye wahitaji humheshimu. 32 Mtu mbaya husukumwa chini katika kutenda mabaya kwake; Bali mwenye haki ana matumaini katika kufa kwake. 33 Hekima hukaa katika moyo wake mwenye ufahamu; Bali yaliyo ndani ya wapumbavu hudhihirika. 34 Haki huinua taifa; Bali dhambi ni aibu ya watu wo wote. 35 Upendeleo wa mfalme humwelekea mtumwa atendaye kwa busara; Bali ghadhabu yake itakuwa juu yake aletaye aibu.