Un clic sur un verset envoie vers le comparateur de versions.
Galates 6.4 Bible en Swahili de l’est
1 Ndugu zangu, mtu akighafilika katika kosa lo lote, ninyi mlio wa Roho mrejezeni upya mtu kama huyo kwa roho ya upole, ukijiangalia nafsi yako usije ukajaribiwa wewe mwenyewe. 2 Mchukuliane mizigo na kuitimiza hivyo sheria ya Kristo. 3 Maana mtu akijiona kuwa ni kitu, naye si kitu, ajidanganya nafsi yake.4 Lakini kila mtu na aipime kazi yake mwenyewe, ndipo atakapokuwa na sababu ya kujisifu ndani ya nafsi yake tu, wala si kwa mwenzake.5 Maana kila mtu atalichukua furushi lake mwenyewe. 6 Mwanafunzi na amshirikishe mkufunzi wake katika mema yote. 7 Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa cho chote apandacho mtu, ndicho atakachovuna. 8 Maana yeye apandaye kwa mwili wake, katika mwili wake atavuna uharibifu; bali yeye apandaye kwa Roho, katika Roho atavuna uzima wa milele. 9 Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho. 10 Kwa hiyo kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema; na hasa jamaa ya waaminio. 11 Tazameni ni kwa herufi gani kubwa nimewaandikia kwa mkono wangu mimi mwenyewe! 12 Wote watakao kuonekana ni wazuri kwa mambo ya mwili, ndio wanaowashurutisha kutahiriwa; makusudi wasiudhiwe kwa ajili ya msalaba wa Kristo, hilo tu. 13 Kwa maana hata wao wenyewe waliotahiriwa hawaishiki sheria; bali wanataka ninyi mtahiriwe, wapate kuona fahari katika miili yenu. 14 Lakini mimi, hasha, nisione fahari juu ya kitu cho chote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambao kwa huo ulimwengu umesulibishwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu. 15 Kwa sababu kutahiriwa si kitu, wala kutokutahiriwa, bali kiumbe kipya. 16 Na wote watakaoenenda kwa kanuni hiyo, amani na iwe kwao na rehema, naam, kwa Israeli wa Mungu. 17 Tangu sasa mtu asinitaabishe; kwa maana ninachukua mwilini mwangu chapa zake Yesu. 18 Ndugu zangu, neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na iwe pamoja na roho zenu. Amina.