Un clic sur un verset envoie vers le comparateur de versions.
Job 11.11 Bible en Swahili de l’est
1 Ndipo Sofari Mnaamathi akajibu, na kusema, 2 Je! Huu wingi wa maneno usijibiwe? Na mtu aliyejaa maneno, je! Ahesabiwe kuwa na haki? 3 Je! Majivuno yako yawanyamazishe watu wawe kimya? Nawe hapo ufanyapo dhihaka, je! Hapana mtu atakayekutahayarisha? 4 Kwa kuwa wewe wasema, Mafunzo yangu ni safi, Nami ni safi machoni pako. 5 Lakini, laiti Mungu angenena, Na kuifunua midomo yake juu yako; 6 Tena akuonyeshe hizo siri za hekima, Ya kuwa hufanikiwa katika kuyatimiza makusudi yake! Ujue basi ya kuwa Mungu akuachilia katika uovu wako. 7 Je! Wewe waweza kuuvumbua ukuu wa Mungu? Waweza kuufikilia upeo wa huyo Mwenyezi? 8 Ni juu mno kama mbingu; waweza kufanya nini wewe? Ni wenye kina kuliko kuzimuni; waweza kujua nini wewe? 9 Cheo chake ni kirefu kuliko dunia, Ni kipana zaidi ya bahari. 10 Yeye akipita, na kufunga watu, Na kuwaita hukumuni, ni nani basi awezaye kumzuia?11 Kwani yeye awajua watu baradhuli; Huona na uovu pia, hata asipoufikiri.12 Lakini mpumbavu aweza kupata ufahamu, Ingawa mwanadamu huzaliwa kama mtoto wa punda-mwitu. 13 Wewe ukiuweka moyo wako kwa uelekevu, Na kumnyoshea mikono yako; 14 Ikiwa una uovu mkononi mwako, uweke mbali nawe, Wala usikubali upuzi kukaa hemani mwako; 15 Hakika ndipo utakapopata kuinua uso pasipo ila; Naam, utathibitika, wala hutakuwa na hofu; 16 Kwa kuwa utasahau mashaka yako; Utayakumbuka kama maji yaliyokwisha pita; 17 Na maisha yako yatakuwa meupe kuliko adhuhuri; Lijapokuwa ni giza, litakuwa kama alfajiri. 18 Nawe utakuwa salama, kwa sababu kuna matumaini; Naam, utatafuta-tafuta kando yako, na kupumzika katika salama. 19 Tena utalala, wala hapana atakayekutia hofu; Naam, wengi watakutafuta uso wako. 20 Lakini macho ya waovu yataingia kiwi, Nao hawatakuwa na njia ya kukimbilia, Na matumaini yao yatakuwa ni kutoa roho.