Un clic sur un verset envoie vers le comparateur de versions.
Esaïe 2.13 Bible en Swahili de l’est
Gloire future de Jérusalem
1 Hili ni neno aliloliona Isaya mwana wa Amozi katika habari za Yuda na Yerusalemu. 2 Na itakuwa katika siku za mwisho, mlima wa nyumba ya Bwana utawekwa imara juu ya milima, nao utainuliwa juu ya vilima; na mataifa yote watauendea makundi makundi. 3 Na mataifa mengi watakwenda na kusema, Njoni, twende juu mlimani kwa Bwana, nyumbani kwa Mungu wa Yakobo, naye atatufundisha njia zake, nasi tutakwenda katika mapito yake maana katika Sayuni itatoka sheria, na neno la Bwana katika Yerusalemu. 4 Naye atafanya hukumu katika mataifa mengi, atawakemea watu wa kabila nyingi; nao watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu; taifa halitainua upanga juu ya taifa lingine, wala hawatajifunza vita tena kamwe. 5 Enyi wa nyumba ya Israeli, njoni, twende katika nuru ya Bwana.
Jugement des idolâtres et des orgueilleux
6 Maana wewe umewaacha watu wako, nyumba ya Israeli, kwa sababu wamejaa kawaida za mashariki, nao ni wapiga ramli kama Wafilisti, na wanapana mikono na wana wa wageni. 7 Tena nchi yao imejaa fedha na dhahabu, wala hapana mwisho wa hazina zao; tena nchi yao imejaa farasi, wala hapana mwisho wa magari yao. 8 Tena nchi yao imejaa sanamu; huabudu kazi ya mikono yao, vitu vilivyofanywa kwa vidole vyao wenyewe. 9 Mtu mnyonge huinama, na mtu mkubwa hujidhili; kwa hiyo usiwasamehe. 10 Ingia ndani ya jabali; ukajifiche mavumbini mbele za utisho wa Bwana, mbele za utukufu wa enzi yake. 11 Macho ya mwanadamu yaliyoinuka yatashushwa chini, na kiburi cha mwanadamu kitainamishwa, naye Bwana, yeye peke yake, atatukuzwa siku hiyo. 12 Kwa maana kutakuwa siku ya Bwana wa majeshi juu ya watu wote wenye kiburi na majivuno, na juu ya yote yaliyoinuka; nayo yatashushwa chini. 13 Na juu ya mierezi yote ya Lebanoni iliyo mirefu na kuinuka, na juu ya mialoni yote ya Bashani; 14 na juu ya milima mirefu yote, na juu ya vilima vyote vilivyoinuka; 15 na juu ya kila mnara mrefu, na juu ya kila ukuta ulio na boma; 16 na juu ya merikebu zote za Tarshishi, na juu ya kila taswira ipendezayo. 17 Na majivuno ya mwanadamu yatainamishwa, na kiburi cha watu kitashushwa; naye Bwana, yeye peke yake, atatukuzwa siku hiyo. 18 Nazo sanamu zitatoweka kabisa. 19 Na watu wataingia ndani ya pango za majabali, na ndani ya mashimo ya nchi, mbele za utisho wa Bwana na utukufu wa enzi yake, atakapoondoka ili aitetemeshe mno dunia. 20 Siku hiyo kila mtu atazitupilia mbali sanamu zake za fedha, na sanamu zake za dhahabu, walizojifanyia ili kuziabudu, kwa fuko na popo; 21 ili aingie ndani ya pango za majabali, na ndani ya tundu za miamba iliyopasuka, mbele za utisho wa Bwana na utukufu wa enzi yake, atakapoondoka ili aitetemeshe mno dunia. 22 Mwacheni mwanadamu ambaye pumzi yake i katika mianzi ya pua yake; kwa maana hudhaniwaje kuwa ni kitu?