Fermer le panneau de recherche

Appuyez sur Entrée pour rechercher ou ESC pour annuler.

Osée 4.12
Bible en Swahili de l’est


Péché et jugement d’Israël

Reproches contre l’idolâtrie

1 Lisikieni neno la Bwana, enyi wana wa Israeli; kwa maana Bwana ana mateto nao wakaao katika nchi, kwa sababu hapana kweli, wala fadhili, wala kumjua Mungu katika nchi.
2 Hapana neno ila kuapa kwa uongo, na kuvunja ahadi, na kuua, na kuiba, na kuzini; huruka mpaka, na damu hugusana na damu.
3 Kwa ajili ya hayo nchi itaomboleza, na kila mtu akaaye ndani yake atadhoofika, pamoja na wanyama wa kondeni na ndege wa angani; naam, samaki wa baharini pia wataondolewa.
4 Walakini asishindane mtu, wala mtu asikemee; maana watu wako ni kama wao washindanao na kuhani.
5 Na wewe utajikwaa wakati wa mchana, na nabii naye atajikwaa pamoja nawe wakati wa usiku; nami nitamwangamiza mama yako.
6 Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa; kwa kuwa wewe umeyakataa maarifa, mimi nami nitakukataa wewe, usiwe kuhani kwangu mimi; kwa kuwa umeisahau sheria ya Mungu wako, mimi nami nitawasahau watoto wako.
7 Kadiri walivyozidishwa, kwa kadiri iyo hiyo walinitenda dhambi; nami nitageuza utukufu wao kuwa aibu.
8 Hujilisha dhambi ya watu wangu, hujifurahisha moyo kwa uovu wao.
9 Hata itakuwa, kama walivyo watu, ndivyo atakavyokuwa kuhani; nami nitawaadhibu kwa ajili ya njia zao, na kuwalipa kwa matendo yao.
10 Nao watakula, lakini hawatashiba; watafanya zinaa, lakini hawataongezeka; kwa sababu wameacha kumwangalia Bwana.
11 Uzinzi na divai na divai mpya huondoa fahamu za wanadamu.
12 Watu wangu hutaka shauri kwa gongo lao, na fimbo yao huwahubiri mambo; maana roho ya uzinzi imewakosesha, nao wamekwenda kuzini mbali na Mungu wao.
13 Hutoa dhabihu juu ya vilele vya milima, na kufukiza uvumba juu ya vilima, chini ya mialoni na milibua na miela, kwa kuwa uvuli wake ni mwema; kwa sababu hiyo binti zenu huzini, na bibi arusi zenu hufanya uasherati.
14 Sitawaadhibu binti zenu wazinipo, wala bibi arusi zenu wafanyapo uasherati; maana wao wenyewe huenda kando pamoja na wanawake wazinzi, hutoa dhabihu pamoja na makahaba; na watu hawa wasiofahamu wataangamia.
15 Ingawa wewe, Israeli, unafanya uzinzi, lakini asiasi Yuda; nanyi msiende Gilgali wala msipande mpaka Beth-Aveni, wala msiape mkisema, Aishivyo Bwana.
16 Kwa maana Israeli ametenda kwa ukaidi, kama ndama mkaidi; sasa je! Bwana atawalisha kama mwana-kondoo katika mahali penye nafasi!
17 Efraimu amejiungamanisha na sanamu; mwache.
18 Kileo chao kimegeuka kuwa uchungu; huzini daima; wakuu wake hupenda aibu.
19 Upepo umemfunikiza kwa mbawa zake; nao watatahayarika kwa sababu ya dhabihu zao.

Cette Bible est dans le domaine public.