Un clic sur un verset envoie vers le comparateur de versions.
Daniel 1.5 Bible en Swahili de l’est
1 Katika mwaka wa tatu wa kumiliki kwake Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, Nebukadreza mfalme wa Babeli,alikwenda Yerusalemu akauhusuru. 2 Bwana akamtia Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, katika mkono wake, pamoja na baadhi ya vyombo vya nyumba ya Mungu; naye akavichukua mpaka nchi ya Shinari, mpaka nyumba ya mungu wake; akaviingiza vile vyombo katika nyumba ya hazina ya mungu wake. 3 Mfalme akamwambia Ashpenazi, mkuu wa matowashi wake, awalete baadhi ya wana wa Israeli, wa uzao wa kifalme, na wa uzao wa kiungwana; 4 vijana wasio na mawaa, wazuri wa uso, wajuzi wa hekima, werevu kwa sababu ya maarifa yao, wenye kufahamu elimu, watakaoweza kusimama katika jumba la mfalme; tena alimwambia awafundishe elimu ya Wakaldayo, na lugha yao.5 Huyo mfalme akawaagizia posho ya chakula cha mfalme, na ya divai aliyokunywa, akaagiza walishwe hivyo muda wa miaka mitatu; ili kwamba hatimaye wasimame mbele ya mfalme.6 Basi katika hao walikuwapo baadhi ya wana wa Yuda, Danielii, na Hanania, na Mishaeli, na Azaria. 7 Mkuu wa matowashi akawapa majina; alimwita Danielii, Belteshaza; na Hanania akamwita Shadraka; na Mishaeli akamwita Meshaki; na Azaria akamwita Abednego. 8 Lakini Danielii aliazimu moyoni mwake ya kuwa hatajitia unajisi kwa chakula cha mfalme, wala kwa divai aliyokunywa; basi akamwomba yule mkuu wa matowashi ampe ruhusa asijitie unajisi. 9 Basi Mungu alimjalia Danielii kupata kibali na huruma machoni pa huyo mkuu wa matowashi. 10 Mkuu wa matowashi akamwambia Danielii, Mimi namwogopa bwana wangu, mfalme, aliyewaagizia ninyi chakula chenu na kinywaji chenu; kwa nini azione nyuso zenu kuwa hazipendezi kama nyuso za vijana hirimu zenu? Basi kwa kufanya hivyo mtahatirisha kichwa changu mbele ya mfalme. 11 Ndipo Danielii akamwambia yule msimamizi, ambaye mkuu wa matowashi amemweka juu ya Danielii, na Hanania, na Mishaeli, na Azaria, 12 Tafadhali utujaribu sisi watumishi wako muda wa siku kumi; na watupe mtama tule, na maji tunywe. 13 Kisha nyuso zetu zitazamwe mbele yako, na nyuso za wale vijana wanaokula chakula cha mfalme; ukatutendee sisi watumishi wako kadiri ya utakavyoona. 14 Basi akawasikiliza katika jambo hilo, akawajaribu siku kumi. 15 Hata mwisho wa zile siku kumi nyuso zao zilikuwa nzuri zaidi, na miili yao ilikuwa imenenepa zaidi, kuliko wale vijana wote waliokula chakula cha mfalme. 16 Basi yule msimamizi akaiondoa posho yao ya chakula, na ile divai waliyopewa wanywe, akawapa mtama tu. 17 Basi, kwa habari za hao vijana wanne, Mungu aliwapa maarifa na ujuzi katika elimu na hekima; Danielii naye alikuwa na ufahamu katika maono yote, na ndoto. 18 Hata mwisho wa siku zile alizoziagiza mfalme za kuwaingiza, mkuu wa matowashi akawaingiza mbele ya mfalme Nebukadreza. 19 Naye mfalme akazungumza nao; na miongoni mwao wote hawakuonekana waliokuwa kama Danielii, na Hanania, na Mishaeli, na Azaria; kwa hiyo wakasimama mbele ya mfalme. 20 Na katika kila jambo la hekima na ufahamu alilowauliza mfalme, akawaona kuwa walifaa mara kumi zaidi ya waganga na wachawi waliokuwa katika ufalme wake. 21 Tena, Danielii huyo akadumu huko hata mwaka wa kwanza wa mfalme Koreshi.