Un clic sur un verset envoie vers le comparateur de versions.
Romains 10.16 Bible en Swahili de l’est
1 Ndugu zangu, nitakayo sana moyoni mwangu, na dua yangu nimwombayo Mungu, ni kwa ajili yao, ili waokolewe. 2 Kwa maana nawashuhudia kwamba wana juhudi kwa ajili ya Mungu, lakini si katika maarifa. 3 Kwa maana, wakiwa hawaijui haki ya Mungu, na wakitaka kuithibitisha haki yao wenyewe, hawakujitia chini ya haki ya Mungu. 4 Kwa maana Kristo ni mwisho wa sheria, ili kila aaminiye ahesabiwe haki. 5 Kwa maana Musa aliandika juu ya haki itokayo kwa sheria, ya kuwa, Mtu afanyaye hiyo ataishi kwa hiyo. 6 Bali ile haki ipatikanayo kwa imani yanena hivi, Usiseme moyoni mwako, Ni nani atakayepanda kwenda mbinguni? (Yaani, ni kumleta Kristo chini), 7 au, Ni nani atakayeshuka kwenda kuzimuni? (Yaani, ni kumleta Kristo juu, kutoka kwa wafu.) 8 Lakini yanenaje? Lile neno li karibu nawe, katika kinywa chako, na katika moyo wako; yaani, ni lile neno la imani tulihubirilo. 9 Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka. 10 Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu. 11 Kwa maana andiko lanena, Kila amwaminiye hatatahayarika. 12 Kwa maana hakuna tofauti ya Myahudi na Myunani; maana yeye yule ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao; 13 kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la Bwana ataokoka. 14 Basi wamwiteje yeye wasiyemwamini? Tena wamwaminije yeye wasiyemsikia? Tena wamsikieje pasipo mhubiri? 15 Tena wahubirije, wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, Ni mizuri kama nini miguu yao wahubirio habari ya mema!16 Lakini si wote walioitii ile habari njema. Kwa maana Isaya asema, Bwana, ni nani aliyeziamini habari zetu?17 Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo. 18 Lakini nasema, Je! Wao hawakusikia? Naam, wamesikia, Sauti yao imeenea duniani mwote, Na maneno yao hata miisho ya ulimwengu. 19 Lakini nasema, Je! Waisraeli hawakufahamu? Kwanza Musa anena, Nitawatia wivu kwa watu ambao si taifa, Kwa taifa lisilo na fahamu nitawaghadhibisha. 20 Na Isaya anao ujasiri mwingi, asema, Nalipatikana nao wasionitafuta, Nalidhihirika kwao wasioniulizia. 21 Lakini kwa Israeli asema, Mchana kutwa naliwanyoshea mikono watu wasiotii na wakaidi.