Un clic sur un verset envoie vers le comparateur de versions.
1 Jean 3 Bible en Swahili de l’est
1 Tazameni, ni pendo la namna gani alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu; na ndivyo tulivyo. Kwa sababu hii ulimwengu haututambui, kwa kuwa haukumtambua yeye. 2 Wapenzi, sasa tu wana wa Mungu, wala haijadhihirika bado tutakavyokuwa; lakini twajua ya kuwa atakapodhihirishwa, tutafanana naye; kwa maana tutamwona kama alivyo. 3 Na kila mwenye matumaini haya katika yeye hujitakasa, kama yeye alivyo mtakatifu. 4 Kila atendaye dhambi, afanya uasi; kwa kuwa dhambi ni uasi. 5 Nanyi mnajua ya kuwa yeye alidhihirishwa, ili aziondoe dhambi; na dhambi haimo ndani yake. 6 Kila akaaye ndani yake hatendi dhambi; kila atendaye dhambi hakumwona yeye, wala hakumtambua. 7 Watoto wadogo, mtu na asiwadanganye; atendaye haki yuna haki, kama yeye alivyo na haki; 8 atendaye dhambi ni wa Ibilisi; kwa kuwa Ibilisi hutenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi. 9 Kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu uzao wake wakaa ndani yake; wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa kutokana na Mungu. 10 Katika hili watoto wa Mungu ni dhahiri, na watoto wa Ibilisi nao. Mtu ye yote asiyetenda haki hatokani na Mungu, wala yeye asiyempenda ndugu yake. 11 Maana, hii ndiyo habari mliyoisikia tangu mwanzo, kwamba tupendane sisi kwa sisi; 12 si kama Kaini alivyokuwa wa yule mwovu, akamwua ndugu yake. Naye alimwua kwa sababu gani? Kwa sababu matendo yake yalikuwa mabaya, na ya ndugu yake yalikuwa ya haki. 13 Ndugu zangu, msistaajabu, ulimwengu ukiwachukia. 14 Sisi tunajua ya kuwa tumepita toka mautini kuingia uzimani, kwa maana twawapenda ndugu. Yeye asiyependa, akaa katika mauti. 15 Kila amchukiaye ndugu yake ni mwuaji: nanyi mnajua ya kuwa kila mwuaji hana uzima wa milele ukikaa ndani yake. 16 Katika hili tumelifahamu pendo, kwa kuwa yeye aliutoa uhai wake kwa ajili yetu; imetupasa na sisi kuutoa uhai wetu kwa ajili ya hao ndugu. 17 Lakini mtu akiwa na riziki ya dunia, kisha akamwona ndugu yake ni mhitaji, akamzuilia huruma zake, je! Upendo wa Mungu wakaaje ndani yake huyo? 18 Watoto wadogo, tusipende kwa neno, wala kwa ulimi, bali kwa tendo na kweli. 19 Katika hili tutafahamu ya kwamba tu wa kweli, nasi tutaituliza mioyo yetu mbele zake, 20 ikiwa mioyo yetu inatuhukumu; kwa maana Mungu ni mkuu kuliko mioyo yetu naye anajua yote. 21 Wapenzi, mioyo yetu isipotuhukumu, tuna ujasiri kwa Mungu; 22 na lo lote tuombalo, twalipokea kwake, kwa kuwa twazishika amri zake, na kuyatenda yapendezayo machoni pake. 23 Na hii ndiyo amri yake, kwamba tuliamini jina la Mwana wake Yesu Kristo, na kupendana sisi kwa sisi, kama alivyotupa amri. 24 Naye azishikaye amri zake hukaa ndani yake yeye naye ndani yake. Na katika hili tunajua ya kuwa anakaa ndani yetu, kwa huyo Roho aliyetupa.