Un clic sur un verset envoie vers le comparateur de versions.
Esaïe 13.1 Bible en Swahili de l’est
Prophéties sur les nations étrangères
Prophétie sur Babylone
1 Ufunuo juu ya Babeli; maono aliyoyaona Isaya, mwana wa Amozi. 2 Haya! Juu ya mlima usio na miti inueni bendera, wapazieni sauti zenu, wapungieni mkono, kwamba waingie katika malango ya wakuu. 3 Mimi mwenyewe nimewaamuru watu wangu waliowekwa wakfu kwangu, naam, nimewaita watu wangu walio hodari kwa ajili ya hasira yangu, watu wangu wenye kutakabari. 4 Kelele milimani kama kelele za watu wengi sana; kelele za falme za mataifa waliokutana pamoja; Bwana wa majeshi anapanga jeshi kwa vita; 5 watu waliotoka katika nchi iliyo mbali, tokea upande wa mwisho wa mbingu; naam, Bwana na silaha za ghadhabu yake, ili aiangamize nchi yote. 6 Pigeni kelele za hofu; maana siku ya Bwana i karibu; itanyesha kama maangamizi yatokayo kwa Mwenyezi Mungu. 7 Kwa sababu hiyo mikono yote italegea, na moyo wa kila mtu utayeyuka. 8 Nao watafadhaika; watashikwa na utungu na maumivu; watakuwa na utungu kama mwanamke aliye karibu na kuzaa; watakodoleana macho; nyuso zao zitakuwa ni nyuso za moto. 9 Tazama, siku ya Bwana inakuja, siku kali, ya hasira na ghadhabu kuu, ili iifanye nchi kuwa ukiwa, na kuwaharibu watu wake, wenye dhambi, wasikae ndani yake. 10 Maana nyota za mbinguni na matangamano havitatoa nuru yake; jua litatiwa giza wakati wa kucha kwake, na mwezi utaacha nuru yake isiangaze. 11 Nami nitaadhibu ulimwengu kwa sababu ya ubaya wake, na wenye dhambi kwa sababu ya hatia yao; nami nitaikomesha fahari yao wenye kiburi; nami nitayaangusha chini majivuno yao walio wakali; 12 nitafanya wanadamu kuadimika kuliko dhahabu safi, na watu kuliko dhahabu ya Ofiri. 13 Kwa hiyo nitazitetemesha mbingu, na dunia itatikiswa itoke katika mahali pake, kwa sababu ya ghadhabu ya Bwana wa majeshi, na kwa sababu ya siku ya hasira yake kali. 14 Basi, itakuwa kama vile paa aliyetishwa, na kama kondoo wasio na mtu wa kuwakusanya; kila mtu atageukia watu wake; nao watakimbia, kila mtu aende nchi yake mwenyewe. 15 Kila mtu atakayeonekana atatumbuliwa, na kila mtu atakayepatikana ataanguka kwa upanga. 16 Na watoto wao wachanga watavunjwa-vunjwa mbele ya macho yao, nyumba zao zitatekwa nyara, na wake zao watatendwa jeuri. 17 Tazama, nitawaamsha Wamedi juu yao, ambao hawaoni fedha kuwa kitu, wala hawafurahii dhahabu. 18 Na nyuta zao zitawaangusha vijana; wala hawatahurumia mazao ya tumbo; jicho lao halitawahurumia watoto. 19 Na Babeli, huo utukufu wa falme, uzuri wa kiburi cha Wakaldayo, utakuwa kama Sodoma na Gomora hapo Mungu alipoiangamiza. 20 Hautakaliwa na watu tena kabisa, wala watu hawatakaa ndani yake tangu kizazi hata kizazi. Mwarabu hatapiga hema yake huko, wala wachungaji hawatalaza makundi yao huko. 21 Lakini huko watalala hayawani wakali wa nyikani; na nyumba zao zitajaa bundi; mbuni watakaa huko; na majini watacheza huko. 22 Na mbwa-mwitu watalia ndani ya ngome zake; na mbweha ndani ya majumba ya anasa; na wakati wake u karibu kufika, na siku zake hazitaongezeka.