Fermer le panneau de recherche

Appuyez sur Entrée pour rechercher ou ESC pour annuler.

Psaumes 72.7
Bible en Swahili de l’est


La gloire d’un royaume juste

1 Ee Mungu, mpe mfalme hukumu zako, Na mwana wa mfalme haki yako.
2 Atawaamua watu wako kwa haki, Na watu wako walioonewa kwa hukumu.
3 Milima itawazalia watu amani, Na vilima navyo kwa haki.
4 Atawahukumu walioonewa wa watu, Atawaokoa wahitaji, atamseta mwenye kuonea.
5 Watakuogopa wakati wote wa kudumu jua, Na wakati wa kung’aa mwezi kizazi hata kizazi.
6 Atashuka kama mvua juu ya majani yaliyokatwa, Kama manyunyu yainyweshayo nchi.
7 Siku zake yeye, mtu mwenye haki atasitawi, Na wingi wa amani hata mwezi utakapokoma.
8 Na awe na enzi toka bahari hata bahari, Toka Mto hata miisho ya dunia.
9 Wakaao jangwani na wainame mbele zake; Adui zake na warambe mavumbi.
10 Wafalme wa Tarshishi na visiwa na walete kodi; Wafalme wa Sheba na Seba na watoe vipawa.
11 Naam, wafalme wote na wamsujudie; Na mataifa yote wamtumikie.
12 Kwa maana atamkomboa mhitaji aliapo, Na mtu aliyeonewa iwapo hana msaidizi.
13 Atamhurumia aliye dhaifu na maskini, Na nafsi za wahitaji ataziokoa.
14 Atawakomboa nafsi zao na kuonewa na udhalimu, Na damu yao ina thamani machoni pake.
15 Basi na aishi; Na wampe dhahabu ya Sheba; Na wamwombee daima; Na kumbariki mchana kutwa.
16 Na uwepo wingi wa nafaka Katika ardhi juu ya milima; Matunda yake na yawaye-waye kama Lebanoni, Na watu wa mjini wasitawi kama majani ya nchi.
17 Jina lake na lidumu milele, Pindi ling’aapo jua jina lake liwe na wazao; Mataifa yote na wajibariki katika yeye, Na kumwita heri.
18 Na ahimidiwe Bwana, Mungu, Mungu wa Israeli, Atendaye miujiza Yeye peke yake;
19 Jina lake tukufu na lihimidiwe milele; Dunia yote na ijae utukufu wake. Amina na Amina.
20 Maombi ya Daudi mwana wa Yese yamekwisha.

Cette Bible est dans le domaine public.