Un clic sur un verset envoie vers le comparateur de versions.
Deutéronome 27.11 Bible en Swahili de l’est
Bénédictions et malédictions
La loi au mont Ébal
1 Musa na wazee wa Israeli wakawaagiza wale watu wakawaambia, Shikeni maagizo yote niwaagizayo leo. 2 Na iwe, siku mtakayovuka Yordani kwenda nchi akupayo Bwana, Mungu wako, ujisimamishie mawe makubwa, ukayatalize matalizo, 3 uyaandike maneno yote ya torati hii juu yake, utakapokwisha kuvuka; ili upate kuingia nchi akupayo Bwana, Mungu wako, nchi imiminikayo maziwa na asali, kama alivyokuahidi Bwana, Mungu wa baba zako. 4 Na iwe, mtakapokwisha vuka Yordani myasimamishe mawe haya, niwaagizayo hivi leo, katika mlima Ebali, nawe yatalize matalizo. 5 Na huko umjengee madhabahu Bwana, Mungu wako, madhabahu ya mawe, usitumie chombo cha chuma juu yake. 6 Jenga hiyo madhabahu ya Bwana, Mungu wako, kwa mawe yasiyochongwa; ukamtolee Bwana, Mungu wako, sadaka za kuteketezwa juu yake; 7 ufanye na sadaka za amani, ukale huko; nawe furahi mbele za Bwana, Mungu wako. 8 Kisha, andika juu ya mawe hayo maneno ya torati hii yote, waziwazi sana. 9 Musa na makuhani Walawi wakawaambia Israeli wote wakasema, Nyamaza, usikize, Ee Israeli; leo umekuwa watu wa Bwana, Mungu wako. 10 Basi isikize sauti ya Bwana, Mungu wako, ufanye maagizo yake na amri zake nikuagizavyo leo.
Bénédictions et malédictions
11 Musa akawaagiza wale watu siku iyo hiyo, akasema, 12 Hawa na wasimame juu ya mlima wa Gerizimu kwa kuwabarikia watu, mkiisha vuka Yordani; Simeoni, na Lawi, na Yuda, na Isakari, na Yusufu, na Benyamini; 13 na hawa na wasimame juu ya mlima wa Ebali kwa laana; Reubeni, na Gadi, na Asheri, na Zabuloni, na Dani, na Naftali. 14 Kisha Walawi na wajibu, wawaambie watu wote wa Israeli kwa sauti kuu, 15 Na alaaniwe mtu afanyaye sanamu ya kuchonga, au ya kusubu, machukizo kwa Bwana, kazi ya mikono ya fundi, akaisimamisha kwa siri. Na watu wote wajibu, waseme, Amina. 16 Na alaaniwe amdharauye baba yake au mama yake. Na watu wote waseme, Amina. 17 Na alaaniwe aondoaye mpaka wa jirani yake. Na watu wote waseme, Amina. 18 Na alaaniwe ampotezaye kipofu akakosa njia. Na watu wote waseme, Amina. 19 Na alaaniwe apotoaye hukumu ya mgeni, na yatima, na mjane aliyefiliwa na mumewe. Na watu wote waseme, Amina. 20 Na alaaniwe alalaye na mke wa baba yake, kwa kuwa amefunua mavazi ya babaye. Na watu wote waseme, Amina. 21 Na alaaniwe alalaye na mnyama wa aina yo yote. Na watu wote waseme, Amina. 22 Na alaaniwe alalaye na umbu lake, binti ya babaye, au binti ya mamaye. Na watu wote waseme, Amina. 23 Na alaaniwe alalaye na mkwewe, mamaye mkewe. Na watu wote waseme, Amina. 24 Na alaaniwe ampigaye mwenzake kwa siri. Na watu wote waseme Amina. 25 Na alaaniwe atwaaye ujira wa kumwua asiye makosa. Na watu wote waseme, Amina. 26 Na alaaniwe asiyeyaweka imara maneno ya torati hii kwa kuyafanya. Na watu wote waseme, Amina.