Fermer le panneau de recherche

Appuyez sur Entrée pour rechercher ou ESC pour annuler.

2 Chroniques 28.17
Bible en Swahili de l’est


Règne d’Achaz

1 Ahazi alikuwa na umri wa miaka ishirini alipoanza kutawala; akatawala katika Yerusalemu miaka kumi na sita; wala hakufanya yaliyo ya adili machoni pa Bwana, kama Daudi babaye;
2 bali akaziendea njia za wafalme wa Israeli, akawafanyizia mabaali sanamu za kusubu.
3 Tena akafukiza uvumba katika bonde la mwana wa Hinomu, akawateketeza wanawe motoni, sawasawa na machukizo ya mataifa, aliowafukuza Bwana mbele ya wana wa Israeli.
4 Akatoa dhabihu na kufukiza uvumba katika mahali pa juu, na vilimani, na chini ya kila mti wenye majani mabichi.
5 Kwa hiyo Bwana, Mungu wake, akamtia mkononi mwa mfalme wa Shamu; wakampiga, wakachukua wa watu wake wafungwa wengi sana, wakawaleta Dameski. Tena akatiwa mkononi mwa mfalme wa Israeli, aliyempiga mapigo makuu.
6 Kwa kuwa Peka mwana wa Remalia akawaua katika Yuda siku moja watu mia na ishirini elfu, mashujaa wote; kwa sababu walikuwa wamemwacha Bwana, Mungu wa baba zao.
7 Naye Zikri, mtu hodari wa Efraimu, akawaua Maaseya mwana wa mfalme, na Azrikamu mkuu wa nyumba, na Elkana, aliyekuwa wa pili wake mfalme.
8 Wana wa Israeli wakachukua wa ndugu zao wafungwa mia mbili elfu, wanawake, na wana, na binti, pia wakachukua kwao nyara nyingi, wakazileta nyara Samaria.
9 Lakini kulikuwako huko nabii wa Bwana, jina lake aliitwa Odedi; akatoka kuwalaki jeshi waliokuja Samaria, akawaambia, Angalieni, kwa kuwa Bwana, Mungu wa baba zenu, aliwakasirikia Yuda, yeye amewatia mikononi mwenu, nanyi mmewaua kwa ghadhabu iliyofikia mbinguni.
10 Na sasa mwanuia kuwatawala wana wa Yuda na Yerusalemu, wawe kwenu watumwa na wajakazi; lakini ninyi nanyi je! Hamna hatia zenu wenyewe juu ya Bwana, Mungu wenu?
11 Haya, nisikieni mimi basi, mwarudishe wafungwa, mliowachukua mateka wa ndugu zenu; kwa maana ghadhabu ya Bwana iliyo kali i juu yenu.
12 Ndipo wakaondoka juu ya hao waliotoka vitani baadhi ya wakuu wa wana wa Efraimu, Azaria, mwana wa Yohanani, na Berekia mwana wa Meshilemothi, na Yehizkia mwana wa Shalumu, na Amasa mwana wa Hadlai,
13 wakawaambia, Hamtawaleta wafungwa humo; kwa sababu mnayanuia yatakayotutia hatiani mbele za Bwana, kuongeza dhambi zetu, na hatia yetu; maana hatia yetu ni kubwa, na ghadhabu kali ipo juu ya Israeli.
14 Basi watu wenye silaha wakawaacha wafungwa na nyara mbele ya wakuu na kusanyiko lote.
15 Wakaondoka wale watu waliotajwa majina yao, wakawatwaa wafungwa, wakawavika kwa zile nyara wote wao waliokuwa uchi, wakawapa mavazi na viatu, wakawalisha, wakawanywesha, wakawatia mafuta, wakawapandisha waliokuwa dhaifu miongoni mwao juu ya punda wakawaleta Yeriko, mji wa mitende, kwa ndugu zao; kisha wakarudi Samaria.
16 Wakati ule mfalme Ahazi akatuma wajumbe kwa mfalme wa Ashuru ili amsaidie.
17 Kwa kuwa Waedomi walikuwa wamekuja tena, na kuwapiga Yuda, na kuwachukua wafungwa.
18 Wafilisti pia walikuwa wameingia miji ya Shefela, na ya Negebu ya Yuda, nao wameutwaa Beth-shemeshi, na Ayaloni, na Gederothi, na Soko pamoja na miji yake, na Timna pamoja na miji yake, na Gimzo pia na miji yake; wakakaa humo.
19 Kwa maana Bwana aliinamisha Yuda kwa ajili ya Ahazi mfalme wa Israeli; kwa kuwa yeye aliwafanyia Yuda aibu, na kumwasi Bwana mno.
20 Na Tiglath-pileseri mfalme wa Ashuru akamjia, akamfadhaisha, asimtie nguvu kwa lo lote.
21 Kwa maana Ahazi alitwaa sehemu katika nyumba ya Bwana, na katika nyumba ya mfalme, na ya wakuu, akampa mfalme wa Ashuru; asisaidiwe na jambo hilo.
22 Na wakati alipofadhaishwa, akazidi kumwasi Bwana, huyo mfalme Ahazi.
23 Kwani akaitolea dhabihu miungu ya Dameski iliyompiga, akasema, Kwa sababu miungu ya wafalme wa Shamu imewasaidia wao, mimi nitaitolea dhabihu, ili inisaidie mimi. Lakini ndiyo iliyomwangamiza yeye na Israeli wote.
24 Tena Ahazi akakusanya vyombo vyote vya nyumba ya Mungu, akavikata vipande vipande vyombo vya nyumba ya Mungu, akaifunga milango ya nyumba ya Bwana; akajifanyizia madhabahu katika kila pembe ya Yerusalemu.
25 Na katika kila mji wa Yuda akafanya mahali pa juu pa kuifukizia miungu mingine uvumba, akamkasirisha Bwana, Mungu wa babaze.
26 Basi mambo yake yote yaliyosalia, na njia zake zote, za kwanza na za mwisho, tazama, yameandikwa katika kitabu cha wafalme wa Yuda na Israeli.
27 Ahazi akalala na babaze, wakamzika mjini, yaani, Yerusalemu; maana hawakumleta makaburini mwa wafalme wa Israeli; na Hezekia mwanawe akatawala mahali pake.

Cette Bible est dans le domaine public.