Un clic sur un verset envoie vers le comparateur de versions.
Deutéronome 8.15 Bible en Swahili de l’est
Terre promise et reconnaissance
1 Amri hii ninayokuamuru leo mtaishika kuitenda, mpate kuishi na kuongezeka, na kuingia katika nchi ile ambayo Bwana aliwaapia baba zenu; nanyi mtaimiliki. 2 Nawe utaikumbuka njia ile yote Bwana, Mungu wako aliyokuongoza miaka hii arobaini katika jangwa, ili akutweze, kukujaribu kuyajua yaliyo moyoni mwako, kwamba utashika amri zake, au sivyo. 3 Akakutweza, akakuacha uone njaa, akakulisha kwa mana, usiyoijua wewe wala baba zako hawakuijua; apate kukujulisha ya kuwa mwanadamu haishi kwa mkate tu, bali huishi kwa kila litokalo katika kinywa cha Bwana. 4 Mavazi yako hayakuchakaa, wala mguu wako haukuvimba, miaka hiyo arobaini. 5 Nawe fikiri moyoni mwako, ya kuwa kama vile baba amrudivyo mwanawe, ndivyo Bwana, Mungu wako, akurudivyo. 6 Nawe uzishike amri za Bwana, Mungu wako, upate kwenda katika njia zake, na kumcha. 7 Kwa kuwa Bwana, Mungu wako, yuakuingiza katika nchi nzuri, nchi yenye vijito vya maji, na chemchemi, na visima, vibubujikavyo katika mabonde na milima; 8 nchi ya ngano na shayiri, na mizabibu, na mitini, na mikomamanga; nchi ya mizeituni yenye mafuta, na asali; 9 nchi utakayokula mikate humo, pasina shida, hutapungukiwa na kitu ndani yake; nchi ambayo mawe yake ni chuma, na milima yake yafukuka shaba. 10 Nawe utakula ushibe, utamshukuru Bwana, Mungu wako, kwa nchi nzuri aliyokupa. 11 Jihadhari, usije ukamsahau Bwana, Mungu wako, kwa kutozishika amri zake, na hukumu zake, na sheria zake, ninazokuamuru leo. 12 Angalia, utakapokuwa umekula na kushiba, na kujenga nyumba nzuri na kukaa ndani yake; 13 na makundi yako ya ng’ombe na kondoo yatakapoongezeka, na fedha yako na dhahabu yako itakapoongezeka, na kila kitu ulicho nacho kitakapoongezeka; 14 basi hapo moyo wako usiinuke, ukamsahau Bwana, Mungu wako, aliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa; 15 aliyekuongoza katika jangwa lile kubwa lenye kitisho, lenye nyoka za moto na nge, nchi ya kiu isiyokuwa na maji; aliyekutolea maji katika mwamba mgumu, 16 aliyekulisha jangwani kwa mana, wasiyoijua baba zako; apate kukutweza, apate kukujaribu, ili kukutendea mema mwisho wako. 17 Hapo usiseme moyoni mwako, Nguvu zangu na uwezo wa mkono wangu ndio ulionipatia utajiri huo. 18 Bali utamkumbuka Bwana, Mungu wako, maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri; ili alifanye imara agano lake alilowapa baba zako, kama hivi leo. 19 Lakini itakuwa, kama ukimsahau Bwana, Mungu wako, na kuiandama miungu mingine, na kuitumikia na kuiabudu, nawashuhudia leo ya kuwa mtaangamia bila shaka. 20 Kama vile mataifa yale ambayo Bwana anawaangamiza mbele yenu, ndivyo mtakavyoangamia; kwa sababu hamkutaka kuisikiliza sauti ya Bwana, Mungu wenu.