1 Paulo, mfungwa wa Kristo Yesu, na Timotheo aliye ndugu yetu, kwa Filemoni mpendwa wetu, mtenda kazi pamoja nasi,
2 na kwa Afia, ndugu yetu, na kwa Arkipo askari mwenzetu, na kwa kanisa lililo katika nyumba yako.
3 Neema na iwe kwenu, na amani, zitokazo kwa Mungu, Baba yetu, na kwa Bwana Yesu Kristo.
4 Namshukuru Mungu wangu sikuzote, nikikukumbuka katika maombi yangu;
5 nikisikia habari za upendo wako na imani uliyo nayo kwa Bwana Yesu na kwa watakatifu wote;
6 ili kwamba ushirika wa imani yako ufanye kazi yake, katika ujuzi wa kila kitu chema kilicho kwetu, katika Kristo.
7 Maana nalikuwa na furaha nyingi na faraja kwa sababu ya upendo wako, kwa kuwa mioyo ya watakatifu imeburudishwa nawe, ndugu yangu.
8 Kwa hiyo, nijapokuwa nina ujasiri katika Kristo kukuagiza likupasalo;
9 lakini, kwa ajili ya upendo nakusihi, kwa kuwa ni kama nilivyo, Paulo mzee, na sasa mfungwa wa Kristo Yesu pia.
10 Nakusihi kwa ajili ya mtoto wangu niliyemzaa katika vifungo vyangu, yaani, Onesimo;
11 ambaye zamani alikuwa hakufai, bali sasa akufaa sana, wewe na mimi pia;
12 niliyemtuma kwako, yeye mwenyewe, maana ni moyo wangu hasa;
13 ambaye mimi nalitaka akae kwangu, apate kunitumikia badala yako katika vifungo vya Injili. 14 Lakini sikutaka kutenda neno lo lote isipokuwa kwa shauri lako, ili kwamba wema wako usiwe kama kwa lazima, bali kwa hiari.
15 Maana, labda ndiyo sababu alitengwa nawe kwa muda, ili uwe naye tena milele;
16 tokea sasa, si kama mtumwa, bali zaidi ya mtumwa, ndugu mpendwa; kwangu mimi sana, na kwako wewe zaidi sana, katika mwili na katika Bwana.
17 Basi kama ukiniona mimi kuwa mshirika nawe, mpokee huyu kama mimi mwenyewe.
18 Na kama amekudhulumu, au unamwia kitu, ukiandike hicho juu yangu.
19 Mimi Paulo nimeandika kwa mkono wangu mwenyewe, mimi nitalipa. Sikuambii kwamba nakuwia hata nafsi yako.
20 Naam, ndugu yangu, nipate faida kwako katika Bwana; uniburudishe moyo wangu katika Kristo.
21 Kwa kuwa nakuamini kutii kwako ndiyo maana nimekuandikia, nikijua ya kuwa utafanya zaidi ya hayo nisemayo.
22 Na pamoja na hayo uniwekee tayari mahali pa kukaa; maana nataraji ya kwamba kwa maombi yenu mtajaliwa kunipata.
23 Epafra, aliyefungwa pamoja nami katika Kristo Yesu, akusalimu;
24 na Marko, na Aristarko, na Dema, na Luka, watendao kazi pamoja nami.
25 Neema ya Bwana Yesu Kristo na iwe pamoja na roho zenu.