Un clic sur un verset envoie vers le comparateur de versions.
Genèse 45.25 Bible en Swahili de l’est
1 Hapo Yusufu hakuweza kujizuia mbele yao wote waliosimama karibu naye. Akapiga kelele, na kusema, Mwondoeni kila mtu mbele yangu. Wala hakusimama mtu pamoja naye, Yusufu alipojitambulisha kwa nduguze. 2 Akapaza sauti yake akalia, nao Wamisri wakasikia. Watu wa nyumba ya Farao nao wakasikia. 3 Yusufu akawaambia ndugu zake, Mimi ndimi Yusufu; baba yangu angali hai bado? Wala ndugu zake hawakuweza kumjibu, maana waliingiwa na hofu mbele yake. 4 Yusufu akawaambia ndugu zake, Karibuni kwangu; basi, wakakaribia. Akasema, Mimi ni Yusufu, ndugu yenu, ambaye mliniuza kwenda Misri. 5 Basi sasa, msihuzunike, wala msiudhike nafsi zenu, kwa kuniuza huku; maana Mungu alinipeleka mbele yenu kuhifadhi maisha ya watu. 6 Maana miaka hii miwili njaa imekuwa katika nchi, na iko tena miaka mitano isiyo na kulima wala kuvuna. 7 Mungu alinipeleka mbele yenu kuwahifadhia masazo katika nchi, na kuwaokoa ninyi kwa wokovu mkuu. 8 Basi si ninyi mlionipeleka huku, ila Mungu; naye ameniweka kama baba kwa Farao, na bwana katika nyumba yake yote, na mtawala katika nchi yote ya Misri. 9 Fanyeni haraka, mmwendee baba yangu, mkamwambie, Hivi ndivyo asemavyo mwanao Yusufu, Mungu ameniweka kuwa bwana katika Misri yote, basi unishukie, usikawie. 10 Nawe utakaa katika nchi ya Gosheni, utakuwa karibu nami, wewe, na wanao, na wana wa wanao, na wanyama wako, ng’ombe zako, na yote uliyo nayo. Nami nitakulisha huko; 11 maana bado imesalia miaka mitano ya njaa; usije ukaingia katika uhitaji, wewe, na nyumba yako, na yote uliyo nayo. 12 Na tazama, macho yenu yanaona, na macho ya ndugu yangu Benyamini, ya kwamba ni kinywa changu mimi kinachosema nanyi. 13 Nanyi mtamwarifu baba yangu habari za fahari yangu yote katika Misri, na za vyote mlivyoviona; mkafanye haraka kumleta huku baba yangu. 14 Akaanguka shingoni mwa ndugu yake Benyamini, akalia; Benyamini naye akalia shingoni mwake. 15 Akawabusu ndugu zake wote, akalia nao, baada ya hayo, nduguze wakazungumza naye 16 Habari ikasikika nyumbani mwa Farao kusema, Ndugu zake Yusufu wamekuja. Ikawa vema machoni pa Farao, na machoni pa watumwa wake. 17 Farao akamwambia Yusufu, Uwaambie ndugu zako, Fanyeni hivi; wachukuzeni mizigo wanyama wenu, mwondoke mwende nchi ya Kanaani; 18 kisha mkamtwae baba yenu, na watu wa nyumbani mwenu, mkanijie; nami nitawapa mema ya nchi ya Misri, nanyi mtakula unono wa nchi. 19 Nawe umeamriwa; fanyeni hivi, mjitwalie magari katika nchi ya Misri kwa watoto wenu wadogo na wake zenu, mkamchukue baba yenu mje. 20 Wala msivisumbukie vyombo vyenu, maana mema ya nchi yote ya Misri ni yenu. 21 Ndivyo walivyofanya wana wa Israeli. Yusufu akawapa magari kama Farao alivyoamuru, akawapa na chakula cha njiani. 22 Akawapa kila mtu nguo za kubadili; lakini Benyamini, alimpa fedha mia tatu na mavazi matano ya kubadili. 23 Na babaye akampelekea kama hivi, punda kumi waliochukua mema ya Misri, na punda wake kumi waliochukua nafaka, na mikate, na chakula kwa babaye njiani. 24 Akaagana na ndugu zake, wakaenda zao; naye akawaambia, Msigombane njiani.25 Wakatoka Misri, wakafika nchi ya Kanaani kwa Yakobo, baba yao.26 Wakampasha habari, wakisema, Yusufu angali hai; naye ndiye mtawala katika nchi yote ya Misri. Moyo wake ukazimia, kwa sababu hakuwasadiki. 27 Wakamwambia maneno yote ya Yusufu, aliyowaambia; na alipoona magari aliyoyapeleka Yusufu, ili kumchukua, roho ya Yakobo baba yao ikafufuka. 28 Israeli akasema, Yatosha! Yusufu mwanangu angali hai; nitakwenda, nionane naye kabla sijafa.