Un clic sur un verset envoie vers le comparateur de versions.
Psaumes 118.21 Bible en Swahili de l’est
Louange à Dieu pour sa bonté
1 Haleluya. Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, Kwa maana fadhili zake ni za milele. 2 Israeli na aseme sasa, Ya kwamba fadhili zake ni za milele. 3 Mlango wa Haruni na waseme sasa, Ya kwamba fadhili zake ni za milele. 4 Wamchao Bwana na waseme sasa, Ya kwamba fadhili zake ni za milele. 5 Katika shida yangu nalimwita Bwana; Bwana akanijibu akaniweka panapo nafasi. 6 Bwana yuko upande wangu, sitaogopa; Mwanadamu atanitenda nini? 7 Bwana yuko upande wangu, msaidizi wangu, Kwa hiyo nitawaona wanaonichukia wameshindwa. 8 Ni heri kumkimbilia Bwana Kuliko kuwatumainia wanadamu. 9 Ni heri kumkimbilia Bwana. Kuliko kuwatumainia wakuu. 10 Mataifa yote walinizunguka; Kwa jina la Bwana naliwakatilia mbali. 11 Walinizunguka, naam, walinizunguka; Kwa jina la Bwana naliwakatilia mbali. 12 Walinizunguka kama nyuki, Walizimika kama moto wa miibani; Kwa jina la Bwana naliwakatilia mbali. 13 Ulinisukuma sana ili nianguke; Lakini Bwana akanisaidia. 14 Bwana ni nguvu zangu na wimbo wangu, Naye amekuwa wokovu wangu. 15 Sauti ya furaha na wokovu Imo hemani mwao wenye haki; Mkono wa kuume wa Bwana hutenda makuu. 16 Mkono wa kuume wa Bwana umetukuzwa; Mkono wa kuume wa Bwana hutenda makuu. 17 Sitakufa bali nitaishi, Nami nitayasimulia matendo ya Bwana. 18 Bwana ameniadhibu sana, Lakini hakuniacha nife. 19 Nifungulieni malango ya haki, Nitaingia na kumshukuru Bwana. 20 Lango hili ni la Bwana, Wenye haki ndio watakaoliingia. 21 Nitakushukuru kwa maana umenijibu, Nawe umekuwa wokovu wangu. 22 Jiwe walilolikataa waashi Limekuwa jiwe kuu la pembeni. 23 Neno hili limetoka kwa Bwana, Nalo ni ajabu machoni petu. 24 Siku hii ndiyo aliyoifanya Bwana, Tutashangilia na kuifurahia. 25 Ee Bwana, utuokoe, twakusihi; Ee Bwana, utufanikishe, twakusihi. 26 Na abarikiwe yeye ajaye kwa jina la Bwana; Tumewabarikia toka nyumbani mwa Bwana. 27 Bwana ndiye aliye Mungu, Naye ndiye aliyetupa nuru. Ifungeni dhabihu kwa kamba Pembeni mwa madhabahu. 28 Ndiwe Mungu wangu, nami nitakushukuru, Ndiwe Mungu wangu, nami nitakutukuza. 29 Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, Kwa maana fadhili zake ni za milele.