Fermer le panneau de recherche

Appuyez sur Entrée pour rechercher ou ESC pour annuler.

Esaïe 19
Bible en Swahili de l’est


1 Ufunuo juu ya Misri. Tazama, Bwana amepanda juu ya wingu jepesi, anafika Misri; na sanamu za Misri zinatikisika mbele zake, na moyo wa Misri unayeyuka ndani yake. 2 Nami nitawaamsha Wamisri juu ya Wamisri; nao watapigana, kila mtu na ndugu yake, na kila mtu na jirani yake, mji juu ya mji, na ufalme juu ya ufalme. 3 Na roho ya Misri itamwagika kabisa katikati yake, nami nitayabatilisha mashauri yake, nao watakwenda kwa sanamu zao, na kwa waganga, na kwa wapiga ramli, na kwa wachawi. 4 Nami nitawatoa hao Wamisri na kuwatia katika mikono ya bwana mgumu; na mfalme mkali atawatawala; asema Bwana, Bwana wa majeshi. 5 Na maji ya baharini yatapunguka, na huo mto utakauka na kuwa pakavu. 6 Na vijito vya mto vitatoa uvundo, na mifereji ya Misri itakuwa haina maji mengi, itakauka; manyasi na mianzi itanyauka. 7 Vitu vimeavyo karibu na Nile, katika ukingo wa Nile, na vyote vilivyopandwa karibu na Nile vitakauka na kuondolewa na kutoweka. 8 Na wavuvi wataugua, na wote wavuao kwa ndoana watahuzunika, nao watandao jarife juu ya maji watazimia. 9 Tena wao wafanyao kazi ya kuchana kitani watafadhaika, na hao pia wafumao bafta. 10 Na nguzo za nchi zitavunjika vipande vipande, wote wafanyao kazi ya mshahara watahuzunika nafsini mwao. 11 Wakuu wa Soani wamekuwa wapumbavu kabisa; washauri wenye hekima wa Farao, shauri lao limepumbazika; mwawezaje kumwambia Farao, Mimi ni mwana wa wenye hekima, ni mwana wa wafalme wa zamani? 12 Wako wapi, basi, watu wako wenye hekima? Na wakuambie sasa; na wajue mambo aliyokusudia Bwana wa majeshi juu ya Misri. 13 Wakuu wa Soani wamekuwa wapumbavu, wakuu wa Nofu wamedanganyika; na hao walio mawe ya pembeni ya kabila zake wameikosesha Misri. 14 Yeye Bwana ametia roho ya ushupavu katika moyo wa Misri, nao wameikosesha Misri katika matendo yake yote, kama mlevi aendavyo huko na huko akitapika. 15 Wala haitakuwako kazi yo yote katika Misri iwezayo kufanywa, ya kichwa au ya mkia, ya tawi au ya nyasi. 16 Katika siku hiyo Misri itakuwa kama wanawake; itatetemeka na kuogopa kwa sababu ya kutikiswa kwa mkono wa Bwana wa majeshi, autikisao juu yake. 17 Na nchi ya Yuda itakuwa sababu ya utisho kwa Misri; kila mtu atakayeambiwa habari zake ataingiwa na woga, kwa sababu ya kusudi la Bwana wa majeshi, analolikusudia juu yake. 18 Katika siku hiyo itakuwako miji mitano katika nchi ya Misri itumiayo lugha ya Kanaani, na kumwapia Bwana wa majeshi; mji mmoja utaitwa Mji wa uharibifu. 19 Katika siku hiyo itakuwako madhabahu katika nchi ya Misri kwa Bwana, na nguzo mpakani mwake kwa Bwana. 20 Nayo itakuwa ishara na ushuhuda kwa Bwana wa majeshi katika nchi ya Misri; kwa maana watamlilia Bwana kwa sababu ya watu wawaoneao, naye atawapelekea mwokozi mwenye kuwatetea, naye atawaokoa. 21 Na Bwana atajulikana na Misri, na Wamisri watamjua Bwana katika siku hiyo; naam watamtumikia kwa dhabihu na matoleo, nao watamwekea Bwana nadhiri, na kuzitekeleza. 22 Naye Bwana atapiga Misri, akipiga na kuponya; nao wakirudi kwa Bwana, atakubali maombi yao na kuwaponya. 23 Katika siku hiyo itakuwako njia kuu itokayo Misri na kufika hata Ashuru; Mwashuri atafika Misri, na Mmisri atafika Ashuru, na Wamisri wataabudu pamoja na Waashuri. 24 Katika siku hiyo Israeli atakuwa wa tatu pamoja na Misri na Ashuru, watakuwa baraka kati ya dunia; 25 kwa kuwa Bwana wa majeshi amewabariki, akisema, Wabarikiwe watu wangu Misri; na wewe Ashuru, kazi ya mikono yangu; na wewe Israeli, urithi wangu.

Cette Bible est dans le domaine public.