Un clic sur un verset envoie vers le comparateur de versions.
Ezéchiel 10.15 Bible en Swahili de l’est
La gloire de Dieu quitte le temple
1 Ndipo nikaangalia, na tazama, katika anga lililokuwa juu ya vichwa vya makerubi, kulionekana juu yao kana kwamba ni yakuti samawi, kuonekana kama mfano wa kiti cha enzi. 2 Naye akamwambia mtu yule aliyevaa bafta, akasema, Ingia kati ya magurudumu yazungukayo, yaani, chini ya kerubi, ukaijaze mikono yako yote miwili makaa ya moto, toka katikati ya makerubi, ukayamwage juu ya mji. Akaingia ndani mbele ya macho yangu. 3 Basi, makerubi walisimama upande wa kuume wa nyumba, hapo alipoingia mtu yule; nalo wingu likaujaza ua wa ndani. 4 Utukufu wa Bwana ukapaa kutoka kwa kerubi yule, ukasimama juu ya kizingiti cha nyumba; nayo nyumba ikajazwa na lile wingu, na ua ulikuwa umejaa mwangaza wa utukufu wa Bwana. 5 Na sauti ya mabawa ya makerubi ikasikiwa, hata katika ua wa nje, kama sauti ya Mungu Mwenyezi, asemapo. 6 Ikawa, hapo alipomwagiza huyo mtu aliyevaa bafta, akisema, Twaa moto kutoka katikati ya magurudumu yazungukayo katikati ya hao makerubi, akaingia, akasimama karibu na gurudumu moja. 7 Na kerubi yule akanyosha mkono wake toka katikati ya makerubi, kwa moto ule uliokuwa katikati ya makerubi, akatwaa baadhi ya moto ule, akautia katika mikono ya mtu yule aliyevaa bafta; naye akautwaa, akatoka. 8 Kukaonekana katika makerubi mfano wa mkono wa mwanadamu chini ya mabawa yao. 9 Nami nikaangalia, na tazama, yalikuwako magurudumu manne karibu na makerubi, gurudumu moja karibu na kerubi mmoja, na gurudumu lingine karibu na kerubi mwingine; na kuonekana kwa magurudumu kulikuwa kana kwamba ni zabarajadi. 10 Na kuonekana kwake, yote manne yalikuwa na mfano mmoja, kana kwamba gurudumu moja lilikuwa ndani ya gurudumu lingine. 11 Walipokwenda, walikwenda kwa pande zao nne; hawakugeuka walipokwenda, lakini walifuata mpaka mahali pale kilipopaelekea kichwa; hawakugeuka walipokwenda. 12 Na mwili wao mzima, na maungo yao, na mikono yao, na mabawa yao, na magurudumu, wamejaa macho pande zote, hata magurudumu waliyokuwa nayo wale wanne. 13 Na magurudumu hayo yaliitwa Kisulisuli, nami nalisikia. 14 Kila mmoja alikuwa na nyuso nne; uso wa kwanza ulikuwa uso wa kerubi, na uso wa pili ulikuwa uso wa mwanadamu, na uso wa tatu ulikuwa uso wa simba, na uso wa nne ulikuwa uso wa tai. 15 Makerubi wakapaa juu; huyo ndiye kiumbe hai niliyemwona karibu na mto Kebari. 16 Na makerubi walipokwenda, magurudumu yale yalikwenda kando yao; na makerubi walipoinua mabawa yao, wapate kupaa juu kutoka katika dunia, magurudumu yale hayakugeuka wala kutoka kando yao. 17 Waliposimama hao, hayo nayo yalisimama; na walipopaa juu hao, hayo nayo yalipaa juu pamoja nao; maana roho ya huyo kiumbe hai ilikuwa ndani yao. 18 Kisha huo utukufu wa Bwana ukatoka pale juu ya kizingiti cha nyumba, ukasimama juu ya makerubi. 19 Nao makerubi wakainua mabawa yao, wakapaa juu kutoka katika dunia machoni pangu, hapo walipotoka nje, nayo magurudumu yakawa kando yao; wakasimama mahali pa kuingilia pa mlango wa upande wa mashariki wa nyumba ya Bwana; na utukufu wa Mungu wa Israeli ulikuwa juu yao. 20 Huyu ndiye kiumbe hai niliyemwona, chini ya Mungu wa Israeli, karibu na mto Kebari; nikajua ya kuwa hao ni makerubi. 21 Kila mmoja alikuwa na nyuso nne, na kila mmoja alikuwa na mabawa manne; na mifano ya mikono ya mwanadamu ilikuwa chini ya mabawa yao. 22 Na mfano wa nyuso zao, ni nyuso zile zile nilizoziona karibu na mto Kebari; kuonekana kwao, na wao wenyewe; kila mmoja walikwenda mbele moja kwa moja.