Un clic sur un verset envoie vers le comparateur de versions.
Joël 1.14 Bible en Swahili de l’est
Une invasion dévastatrice
1 Neno la Bwana lililomjia Yoeli, mwana wa Pethueli. 2 Sikieni haya, enyi wazee; Sikilizeni, enyi wenyeji wote wa nchi. Je! Mambo haya yamekuwako katika siku zenu, Au katika siku za baba zenu? 3 Waarifuni watoto wenu habari yake, Watoto wenu wakawaambie watoto wao, Na watoto wao wakakiambie kizazi kingine. 4 Yaliyosazwa na tunutu yameliwa na nzige; na yaliyosazwa na nzige yameliwa na parare; na yaliyosazwa na parare yameliwa na madumadu. 5 Levukeni, enyi walevi, mkalie; Pigeni yowe, ninyi nyote mnywao divai; Kwa sababu ya divai mpya; Maana umekatiliwa mbali na vinywa vyenu. 6 Maana taifa limepanda juu ya nchi yangu, Lenye nguvu, tena halina hesabu; Meno yake ni kama meno ya simba, Naye ana magego ya simba mkubwa. 7 Ameuharibu mzabibu wangu; ameuvunja mtini wangu; ameyaambua magamba yake kabisa; ameuangusha chini; matawi yake yamefanywa kuwa meupe. 8 Ombolea kama mwanamwali avaaye magunia Kwa ajili ya mume wa ujana wake. 9 Sadaka ya unga na sadaka ya kinywaji Zimekatiliwa mbali na nyumba ya Bwana; Hao makuhani, wahudumu wa Bwana, wanaomboleza. 10 Shamba limeharibika, nchi inaomboleza; maana nafaka imeharibika, divai mpya imekauka, mafuta yamepunguka. 11 Tahayarini, enyi wakulima; Pigeni yowe, enyi watunzaji wa mizabibu; Kwa ajili ya ngano na shayiri, Maana mavuno ya mashamba yamepotea. 12 Mzabibu umesinyaa, mtini nao umevia; Nao mkomamanga na mtende na mtofaa; Naam, miti yote ya mashamba imekauka; Maana furaha imekauka katika wanadamu. 13 Jikazeni mkaomboleze, enyi makuhani; Pigeni yowe, enyi wahudumu wa madhabahu; Njoni mlale usiku kucha katika magunia, Enyi wahudumu wa Mungu wangu; Kwa kuwa sadaka ya unga na sadaka ya kinywaji Zimezuiwa katika nyumba ya Mungu wenu. 14 Takaseni saumu, iteni kusanyiko la dini, Wazee na wakusanye wenyeji wote wa nchi; Waende nyumbani kwa Bwana, Mungu wenu, Na kumlilia Bwana, 15 Ole wake siku hii! Kwa maana siku ya Bwana inakaribia, nayo itakuja kama uangamivu utokao kwake aliye Mwenyezi. 16 Je! Chakula hakikukatiliwa mbali mbele ya macho yetu? Naam, furaha na kicheko mbali na nyumba ya Mungu wetu? 17 Mbegu zinaoza chini ya udongo wake; ghala zimeachwa ukiwa; mabanda yamevunjika; kwa maana nafaka imekauka. 18 Jinsi wanyama wanavyougua! Makundi ya ng’ombe yamefadhaika, kwa sababu hawana malisho; naam, makundi ya kondoo yamepata mateso. 19 Ee Bwana, nakulilia wewe; Kwa maana moto umeyala malisho ya nyikani, Na miali ya moto imeteketeza miti yote ya mashamba. 20 Naam, wanyama wa mashamba wanakutwetea wewe; Kwa maana vijito vya maji vimekauka, Na moto umeyateketeza malisho ya nyikani.