Un clic sur un verset envoie vers le comparateur de versions.
Habakuk 3.16 Bible en Swahili de l’est
Cantique d’Habakuk
1 Sala ya nabii Habakuki. 2 Ee Bwana, nimesikia habari zako, nami naogopa; Ee Bwana, fufua kazi yako katikati ya miaka; Katikati ya miaka tangaza habari yake; Katika ghadhabu kumbuka rehema. 3 Mungu alikuja kutoka Temani, Yeye aliye mtakatifu kutoka mlima Parani. Utukufu wake ukazifunika mbingu, Nayo dunia ikajaa sifa yake. 4 Mwangaza wake ulikuwa kama nuru; Alikuwa na mishale ya nuru ubavuni pake; Ndipo ulipofichwa uweza wake. 5 Mbele zake ilikwenda tauni, Na makaa ya moto yakatoka miguuni pake. 6 Akasimama, akaitetemesha dunia; Akatazama, akawasitusha mataifa; Na milima ya zamani ikatawanyika; Vilima vya kale vikainama; Miendo yake ilikuwa kama siku za kale. 7 Naliziona hema za Kushani katika taabu; Mapazia ya nchi ya Midiani yakatetemeka. 8 Je! Bwana aliikasirikia mito? Je! Hasira yako ilikuwa juu ya mito, Au ghadhabu yako juu ya bahari, Hata ukapanda farasi zako, Katika magari yako ya wokovu? 9 Uta wako ukafanywa wazi kabisa; Viapo walivyopewa kabila vilikuwa neno thabiti; Ukaipasua nchi kwa mito. 10 Milima ilikuona, ikaogopa; Gharika ya maji ikapita; Vilindi vikatoa sauti yake, Vikainua juu mikono yake. 11 Jua na mwezi vikasimama makaoni mwao; Mbele ya nuru ya mishale yako ilipotapakaa, Mbele ya mwangaza wa mkuki wako umeremetao. 12 Ulikwenda katikati ya nchi kwa ghadhabu; Ukawapura mataifa kwa hasira. 13 Ukatokea kwa ajili ya wokovu wa watu wako, Kwa ajili ya wokovu wa masihi wako; Ukakiponda kichwa cha nyumba ya waovu, Ukiuweka wazi msingi hata mwambani. 14 Ukakichoma kichwa cha mashujaa wake kwa fimbo zao wenyewe; Wakaja kama kisulisuli ili kunitawanya; Kama wakifurahi kuwameza maskini kwa siri. 15 Ukaikanyaga bahari kwa farasi zako, Chungu ya maji yenye nguvu. 16 Nikasikia, na tumbo langu likatetemeka, Midomo yangu ikatikisika kwa sauti ile; Ubovu ukaingia mifupani mwangu, Nikatetemeka katika mahali pangu; Ili nipate kuingoja ile siku ya dhiki, Kundi lao washambuliao wakweapo juu ya watu. 17 Maana mtini hautachanua maua, Wala mizabibuni hamtakuwa na matunda; Taabu ya mzeituni itakuwa bure, Na mashamba hayatatoa chakula; Zizini hamtakuwa na kundi, Wala vibandani hamtakuwa na kundi la ng’ombe; 18 Walakini nitamfurahia Bwana Nitamshangilia Mungu wa wokovu wangu. 19 YEHOVA, aliye Bwana, ni nguvu zangu, Yeye huifanya miguu yangu kuwa kama ya kulungu, Naye ataniendesha katika mahali pangu palipoinuka.