Un clic sur un verset envoie vers le comparateur de versions.
Job 37.15 Bible en Swahili de l’est
1 Moyo wangu hunitetema kwayo pia, Nao hutoka mahali pake. 2 Zisikizeni hizo kelele za sauti yake, Na uvumi utokao kinywani mwake. 3 Yeye huituma iende chini ya mbingu zote, Na radi yake hata miisho ya nchi. 4 Baadaye sauti hunguruma; Yeye hunguruma kwa sauti ya ukuu wake; Hazizuii hapo sauti yake isikiwapo. 5 Mungu hunguruma kwa kustaajabisha kwa sauti yake; Hufanya mambo makuu, ambayo hatuwezi kuelewa nayo. 6 Kwani huiambia theluji, Anguka juu ya nchi; Na vivyo manyonyota ya mvua, Na hayo maji ya mvua yake kubwa. 7 Huufunga mkono wa kila binadamu; Ili watu wote aliowaumba wajue. 8 Hapo wanyama huingia mafichoni, Na kukaa katika mapango yao. 9 Dhoruba hutoka katika vyumba vyake; Na baridi ghalani mwake. 10 Barafu huletwa kwa pumzi za Mungu; Na upana wa maji huganda. 11 Naam, huyatweka mawingu mazito mzigo wa maji; Hulitandika wingu la umeme wake; 12 Nalo hugeuzwa huku na huku kwa uongozi wake, Ili yafanye yote atakayoyaagiza Juu ya uso wa dunia hii ikaayo watu; 13 Kama ni kwa kuonya, au kama ni kwa nchi yake, Au kama ni kwa rehema, ndiye aletaye. 14 Sikiliza neno hili, Ee Ayubu; Simama kimya, uzifikiri kazi za Mungu za ajabu. 15 Je! Wajua wewe jinsi Mungu anavyoziagiza, Na kuumulikisha umeme wa wingu lake? 16 Je! Wajua jinsi mawingu yalivyowekwa sawasawa, Hizo kazi za ajabu za huyo mkamilifu wa maarifa? 17 Jinsi nguo zako zilivyo na moto, Hapo nchi ituliapo kwa sababu ya upepo wa kusini? 18 Je! Waweza kuzitandaza mbingu pamoja naye, Ambazo zina nguvu kama kioo cha kuyeyushwa? 19 Utufundishe ni maneno gani tutakayomwambia; Kwa maana hamwezi kuyatengeza kwa sababu ya giza. 20 Je! Aambiwe kwamba nataka kunena? Au mtu angetamani kumezwa? 21 Na sasa watu hawawezi kuutazama mwanga ung’aao mbinguni; Lakini upepo ukipita huzitakasa. 22 Kaskazini hutokea umemetufu wa dhahabu; Mungu huvikwa ukuu utishao. 23 yeye Mwenyezi hamwezi kumwona; Yeye ni mkuu mwenye uweza; Tena mwenye hukumu, na mwingi wa haki, hataonea. 24 Kwa hiyo watu humwogopa; Yeye hawaangalii walio na hekima mioyoni.