Fermer le panneau de recherche

Appuyez sur Entrée pour rechercher ou ESC pour annuler.

Psaumes 102.19
Bible en Swahili de l’est


Prière dans la détresse

1 Ee Bwana, usikie kuomba kwangu, Kilio changu kikufikie.
2 Usinifiche uso wako siku ya shida yangu, Unitegee sikio lako, siku niitapo unijibu upesi.
3 Maana siku zangu zinatoweka kama moshi, Na mifupa yangu inateketea kama kinga.
4 Moyo wangu umepigwa kama majani na kukauka, Naam, ninasahau kula chakula changu.
5 Kwa ajili ya sauti ya kuugua kwangu Mifupa yangu imegandamana na nyama yangu.
6 Nimekuwa kama mwari nyuni wa jangwani, Na kufanana na bundi wa mahameni.
7 Nakesha, tena nimekuwa kama shomoro Aliye peke yake juu ya nyumba.
8 Adui zangu wananilaumu mchana kutwa; Wanaonichukia kana kwamba wana wazimu Huapa kwa kunitaja mimi.
9 Maana nimekula majivu kama chakula, Na kukichanganya kinywaji changu na machozi.
10 Kwa sababu ya ghadhabu yako na hasira yako; Maana umeniinua na kunitupilia mbali.
11 Siku zangu zi kama kivuli kilichotandaa, Nami ninanyauka kama majani.
12 Bali Wewe, Bwana utaketi ukimiliki milele, Na kumbukumbu lako kizazi hata kizazi.
13 Wewe mwenyewe utasimama, Na kuirehemu Sayuni, Kwa maana ndio wakati wa kuihurumia, Naam, majira yaliyoamriwa yamewadia.
14 Maana watumishi wako wameyaridhia mawe yake, Na kuyaonea huruma mavumbi yake.
15 Kisha mataifa wataliogopa jina la Bwana, Na wafalme wote wa dunia utukufu wako;
16 Bwana atakapokuwa ameijenga Sayuni, Atakapoonekana katika utukufu wake,
17 Atakapoyaelekea maombi yake aliye mkiwa, Asiyadharau maombi yao.
18 Kizazi kitakachokuja kitaandikiwa hayo, Na watu watakaoumbwa watamsifu Bwana.
19 Maana ametazama toka patakatifu pake pa juu, Toka mbinguni Bwana ameiangalia nchi,
20 Ili akusikie kuugua kwake aliyefungwa, Na kuwafungua walioandikiwa kufa.
21 Watu walitangaze jina la Bwana katika Sayuni, Na sifa zake katika Yerusalemu,
22 Pindi mataifa watapokusanyika pamoja, Falme nazo ili kumtumikia Bwana.
23 Amezipunguza nguvu zangu njiani; Amezifupisha siku zangu.
24 Nitasema, Ee Mungu wangu, usiniondoe katikati ya siku zangu; Miaka yako ni tangu kizazi hata kizazi.
25 Hapo mwanzo uliutia msingi wa nchi, Na mbingu ni kazi ya mikono yako.
26 Hizi zitaharibika, bali Wewe utadumu Naam, hizi zitachakaa kama nguo; Na kama mavazi utazibadilisha, Nazo zitabadilika.
27 Lakini Wewe U Yeye yule; Na miaka yako haitakoma.
28 Wana wa watumishi wako watakaa, Na wazao wao wataimarishwa mbele zako.

Cette Bible est dans le domaine public.