Un clic sur un verset envoie vers le comparateur de versions.
Actes 25.26 Bible en Swahili de l’est
Paul devant le gouverneur Festus
1 Hata Festo alipokwisha kuingia katika uliwali, baada ya siku tatu akapanda kwenda Yerusalemu kutoka Kaisaria. 2 Kuhani Mkuu na wakuu wa Wayahudi wakampasha habari za Paulo, wakamsihi, 3 na kumwomba fadhili juu yake, kwamba atoe amri aletwe Yerusalemu, wapate kumwotea na kumwua njiani. 4 Lakini Festo akajibu ya kwamba Paulo analindwa Kaisaria; naye mwenyewe yu tayari kwenda huko karibu. 5 Akasema, Wale walio na mamlaka kwenu na watelemke pamoja nami wakamshitaki, ikiwa liko neno baya katika mtu huyu. 6 Alipokwisha kukaa kwao siku nane au kumi si zaidi, akatelemkia Kaisaria; hata siku ya pili akaketi katika kiti cha hukumu akaamuru Paulo aletwe. 7 Alipokuja, wale Wayahudi walioshuka kutoka Yerusalemu wakasimama karibu yake wakaleta mashitaka mengi mazito juu yake, wasiyoweza kuyayakinisha. 8 Paulo akasema akijitetea, Mimi sikukosa neno juu ya sheria ya Wayahudi, wala juu ya hekalu, wala juu ya Kaisari. 9 Lakini Festo akitaka kujipendekeza kwa Wayahudi akamjibu Paulo, akisema, Je! Wataka kwenda Yerusalemu, ukahukumiwe huko mbele yangu kwa ajili ya mambo hayo? 10 Paulo akasema, Mimi ninasimama hapa mbele ya kiti cha hukumu cha Kaisari, ndipo panipasapo kuhukumiwa; sikuwakosa Wayahudi neno, kama wewe ujuavyo sana. 11 Basi ikiwa ni mkosa au nimetenda neno la kustahili kufa, sikatai kufa; bali, kama si kweli neno hili wanalonishitaki, hapana awezaye kunitia mikononi mwao. Nataka rufani kwa Kaisari. 12 Basi Festo alipokwisha kusema na watu wa baraza, akajibu, Umetaka rufani kwa Kaisari! Basi, utakwenda kwa Kaisari. 13 Siku kadha wa kadha zilipokwisha kupita, Agripa mfalme na Bernike wakafika Kaisaria, wakimwamkia Festo. 14 Na walipokuwa wakikaa huko siku nyingi, Festo akamweleza mfalme habari za Paulo, akisema, Yupo hapa mtu mmoja aliyeachwa na Feliki kifungoni; 15 ambaye nilipokuwa Yerusalemu wakuu wa makuhani na wazee wa Wayahudi wakaniarifu habari zake, wakinitaka hukumu juu yake. 16 Nikawajibu kwamba si desturi ya Warumi kumtoa mtu awaye yote, kabla mtu yule aliyeshitakiwa hajaonana na washitaki wake uso kwa uso, na kupewa nafasi ya kujitetea katika mashitaka yake. 17 Basi walipokutanika hapa sikukawia; bali siku ya pili nikaketi katika kiti cha hukumu nikaamuru mtu huyo aletwe. 18 Na wale waliomshitaki waliposimama hawakuleta neno lo lote baya, kama nilivyodhani, 19 bali walikuwa na maswali mengine mengine juu yake katika dini yao wenyewe, na katika habari ya mtu mmoja Yesu, aliyekuwa amekwisha kufa, ambaye Paulo alikaza kusema kwamba yu hai. 20 Nami nikaona shaka jinsi ya kutafuta hakika ya habari hii, nikamwuliza kama anataka kwenda Yerusalemu ahukumiwe huko katika mambo haya. 21 Lakini Paulo alipodai kuwekwa ahukumiwe na Kaisari, nikaamuru alindwe hata nitakapompeleka kwa Kaisari. 22 Agripa akamwambia Festo, Mimi nami nalikuwa nikitaka kumsikia mtu huyu. Akasema, Utamsikia kesho. 23 Hata asubuhi Agripa akaja pamoja na Bernike kwa fahari nyingi, wakaingia mahali pa kusikia maneno, pamoja na maakida wakuu na watu wakuu wa mji; Festo akatoa amri, Paulo akaletwa. 24 Festo akasema, Mfalme Agripa, na ninyi nyote mliopo hapa pamoja nasi, mnamwona mtu huyu, ambaye jamii yote ya Wayahudi huko Yerusalemu na hapa pia wamenitaka niwasaidie, wakipiga kelele kwamba haimpasi kuishi zaidi. 25 Lakini mimi naliona kwamba hakutenda neno la kustahili kuuawa, na yeye mwenyewe alipotaka kuhukumiwa na Kaisari, nalikusudia kumpeleka kwake. 26 Nami katika habari yake sina neno la hakika la kumwandikia bwana. Kwa hiyo nimemleta hapa mbele yenu, hasa mbele yako wewe, mfalme Agripa, ili akiisha kuulizwa-ulizwa nipate neno la kuandika. 27 Kwa maana naona ni neno lisilo maana kumpeleka mfungwa, bila kuonyesha mashitaka yale aliyoshitakiwa.