Fermer le panneau de recherche

Appuyez sur Entrée pour rechercher ou ESC pour annuler.

Psaumes 73.18
Bible en Swahili de l’est


1 Hakika Mungu ni mwema kwa Israeli, Kwa hao walio safi mioyo yao. 2 Nami miguu yangu ilikuwa karibu na kupotoka, Hatua zangu zilikuwa karibu na kuteleza. 3 Maana naliwaonea wivu wenye kujivuna, Nilipoiona hali ya amani ya wasio haki. 4 Maana hawana maumivu katika kufa kwao, Na mwili wao una nguvu. 5 Katika taabu ya watu hawamo, Wala hawapati mapigo pamoja na wanadamu. 6 Hivyo kiburi kimekuwa mkufu shingoni mwao, Jeuri huwavika kama nguo. 7 Macho yao hutokeza kwa kunenepa, Wameipita kadiri ya mawazo ya mioyo yao. 8 Hudhihaki, husimulia mabaya, Husimulia udhalimu kana kwamba wako juu. 9 Wameweka kinywa chao mbinguni, Na ulimi wao hutanga-tanga duniani. 10 Kwa hiyo watu wake hugeuka huko, Na maji yaliyojaa humezwa nao. 11 Nao husema, Mungu ajuaje? Yako maarifa kwake aliye juu? 12 Fahamu, ndivyo walivyo wasio haki, Na kwa kustarehe sikuzote wamepata mali nyingi. 13 Hakika nimejisafisha moyo wangu bure, Nimenawa mikono yangu kwa kutokukosa. 14 Maana mchana kutwa nimepigwa, Na kuadhibiwa kila asubuhi. 15 Kama ningalisema, Nitasimulia kama hayo; Kumbe! Ningaliwadanganya kizazi cha wana wako. 16 Nami nalifikiri jinsi ya kufahamu hayo; Ikawa taabu machoni pangu; 17 Hata nilipoingia katika patakatifu pa Mungu, Nikautafakari mwisho wao. 18 Hakika Wewe huwaweka penye utelezi, Huwaangusha mpaka palipoharibika. 19 Namna gani wamekuwa ukiwa mara! Wametokomea na kutoweshwa kwa utisho. 20 Ee Bwana, kama ndoto wakati wa kuamka, Uondokapo utaidharau sanamu yao. 21 Moyo wangu ulipoona uchungu, Viuno vyangu viliponichoma, 22 Nalikuwa kama mjinga, sijui neno; Nalikuwa kama mnyama tu mbele zako. 23 Walakini mimi ni pamoja nawe daima, Umenishika mkono wa kuume. 24 Utaniongoza kwa shauri lako, Na baadaye utanikaribisha kwa utukufu. 25 Ni nani niliye naye mbinguni, Wala duniani sina cha kupendeza ila Wewe. 26 Mwili wangu na moyo wangu hupunguka, Bali Mungu ni mwamba wa moyo wangu Na sehemu yangu milele. 27 Maana wajitengao nawe watapotea; Umewaangamiza wote waliokuacha Wewe. 28 Nami kumkaribia Mungu ni kwema kwangu; Nimefanya kimbilio kwa Bwana MUNGU, Niyahubiri matendo yako yote.

Cette Bible est dans le domaine public.