Un clic sur un verset envoie vers le comparateur de versions.
Proverbes 11.29 Bible en Swahili de l’est
1 Mizani ya hadaa ni chukizo kwa Bwana; Bali vipimo vilivyo sawasawa humpendeza. 2 Kijapo kiburi ndipo ijapo aibu; Bali hekima hukaa na wanyenyekevu. 3 Ukamilifu wao wenye haki utawaongoza Bali ukaidi wao wenye fitina utawaangamiza. 4 Mali hazifaidii kitu siku ya ghadhabu; Bali haki huokoa na mauti. 5 Haki yake mtu mkamilifu itamwongoza njia yake; Bali mtu mwovu ataanguka kwa uovu wake. 6 Haki yao wenye haki itawaokoa; Bali wafanyao fitina watanaswa kwa hila yao wenyewe. 7 Mtu mwovu atakapokufa, taraja lake lapotea; Na matumaini ya uovu huangamia. 8 Mwenye haki huokolewa katika dhiki, Na mtu mwovu ataiingia badala yake. 9 Asiyemcha Mungu humpoteza jirani yake kwa kinywa chake; Bali wenye haki watapona kwa maarifa. 10 Wenye haki wasitawipo, mji hufurahi; Waovu waangamiapo, watu hupiga kelele. 11 Mji hutukuzwa kwa mbaraka wa mwenye haki; Bali mji hupinduliwa kwa kinywa cha mwovu. 12 Asiye na akili humdharau mwenziwe; Bali mtu aliye na ufahamu hunyamaza. 13 Mwenye kitango akisingizia hufunua siri; Bali mwenye roho ya uaminifu husitiri mambo. 14 Pasipo mashauri taifa huanguka; Bali kwa wingi wa washauri huja wokovu. 15 Amdhaminiye mgeni hakosi ataumia; Achukiaye mambo ya dhamana yu salama. 16 Mwanamke wa adabu huheshimiwa daima; Na watu wakali hushika mali siku zote. 17 Mwenye rehema huitendea mema nafsi yake; Aliye mkali hujisumbua mwili wake. 18 Mtu mwovu hupata mshahara wa udanganyifu; Apandaye haki ana thawabu ya hakika. 19 Haki huelekea uzima; Afuataye maovu hufuata mauti yake mwenyewe. 20 Wenye kuhalifu moyoni ni chukizo kwa Bwana; Walio wakamilifu katika njia zao humpendeza. 21 Hakika, mtu mwovu hatakosa adhabu; Bali wazao wa wenye haki wataokoka. 22 Kama pete ya dhahabu katika pua ya nguruwe, Kadhalika mwanamke mzuri asiye na akili. 23 Haja ya mwenye haki ni mema tu; Bali kutaraji kwake mtu mwovu ni ghadhabu. 24 Kuna atawanyaye, lakini huongezewa zaidi; Kuna azuiaye isivyo haki, lakini huelekea uhitaji. 25 Nafsi ya mtu mkarimu itawandishwa; Anyweshaye atanyweshwa mwenyewe. 26 Awanyimaye watu nafaka, watu watamlaani; Auzaye nafaka, baraka itakuwa kichwani pake. 27 Atafutaye mema kwa bidii hutafuta fadhili; Atafutaye madhara, hayo yatamjia. 28 Azitegemeaye mali zake ataanguka; Mwenye haki atasitawi kama jani. 29 Ataabishaye nyumba yake mwenyewe ataurithi upepo; Mpumbavu atakuwa mtumwa wa mtu mwenye moyo wa akili. 30 Mazao ya mwenye haki ni mti wa uzima; Na mwenye hekima huvuta roho za watu. 31 Tazama, mwenye haki atalipwa duniani; Basi mwovu na mkosaji si mara nyingi zaidi?