Un clic sur un verset envoie vers le comparateur de versions.
Esaïe 22.20 Bible en Swahili de l’est
1 Ufunuo juu ya bonde la maono. Sasa una nini, wewe, Hata umepanda pia juu ya dari za nyumba? 2 Ewe uliyejaa makelele, Mji wa ghasia, mji wenye furaha; Watu wako waliouawa hawakuuawa kwa upanga, Wala hawakufa vitani. 3 Wakuu wako wote wamekimbia pamoja, Wamefungwa wasiutumie upinde. Wote walioonekana wamefungwa pamoja, Wamekimbia mbali sana. 4 Kwa sababu hiyo nasema, Geuza uso wako usinitazame, nipate kulia kwa uchungu; usijishughulishe kunifariji, kwa ajili ya kuharibika kwake binti ya watu wangu. 5 Kwa maana siku ya kutaabika, siku ya kukanyagwa, siku ya fujo inakuja, itokayo kwa Bwana, Bwana wa majeshi, katika bonde la Maono; inabomoa kuta; na kuililia milima. 6 Na Elamu wameshika podo, pamoja na magari ya vita, na watu wenye kupanda farasi; na Kiri wameifunua ngao. 7 Hata ikawa mabonde yako mateule yamejaa magari ya vita, nao wapandao farasi wamejipanga wakielekea malango. 8 Kisha alikiondoa kifuniko cha Yuda, nawe siku hiyo ulivitazama vyombo vya vita katika nyumba ya mwituni. 9 Nanyi mlipaona mahali palipobomoka katika mji wa Daudi ya kuwa ni pengi, nanyi mliyakusanya maji ya birika la chini. 10 Nanyi mlizihesabu nyumba za Yerusalemu, mkazibomoa nyumba ili kuutia nguvu ukuta. 11 Nanyi mlifanya birika la maji katikati ya kuta mbili, la kuwekea maji ya birika la kale; lakini hamkumwangalia yeye aliyeyafanya hayo, wala kumjali yeye aliyeyatengeneza zamani. 12 Siku hiyo Bwana, Bwana wa majeshi, akawaita watu walie na kuomboleza, na kung’oa nywele zao, na kuvaa nguo za magunia; 13 na kumbe! Furaha, na kuchekelea, na kuchinja ng’ombe, na kuchinja kondoo, na kula nyama, na kunywa mvinyo; tule, tunywe, kwa maana kesho tutakufa. 14 Na yeye Bwana wa majeshi akafunua haya masikioni mwangu, Ni kweli, uovu huu hautatakaswa wala kuwatokeni hata mfe; asema Bwana, Bwana wa majeshi. 15 Bwana, Bwana wa majeshi, asema hivi, Haya! Enenda kwa huyu mtunza hazina, yaani, Shebna, aliye juu ya nyumba, ukamwambie, 16 Unafanyaje hapa? Nawe una nani hapa? Hata ukachimba kaburi hapa; ukamchimbia kaburi huko juu, na kumchongea makao katika jabali! 17 Tazama, Bwana atakutupa kwa nguvu, kama mtu mwenye nguvu; naam, atakuzonga-zonga. 18 Hakika atakukunja na kukutupa kama mpira, mpaka nchi iliyo mbali; huko utakufa, na magari ya utukufu wako yatakuwa kuko huko, ewe uliye aibu ya nyumba ya bwana wako. 19 Nami nitakusukuma na kukutoa katika mahali pako, naye atakushusha utoke hapa usimamapo.20 Na itakuwa katika siku ile nitamwita mtumishi wangu Eliakimu, mwana wa Hilkia;21 nami nitamvika vazi lako, nitamtia nguvu kwa mshipi wako, nami nitamkabidhi yeye mamlaka yako; naye atakuwa baba kwa wenyeji wa Yerusalemu, na kwa nyumba ya Yuda. 22 Na ufunguo wa nyumba ya Daudi nitauweka begani mwake; yeye atafungua wala hapana atakayefunga; naye atafunga wala hapana atakayefungua. 23 Nami nitamkaza kama msumari mahali palipo imara; naye atakuwa kiti cha utukufu kwa nyumba ya baba yake. 24 Nao wataangika juu yake utukufu wote wa nyumba ya baba yake; wazao wake na watoto wao, kila chombo kidogo tangu vyombo vya vikombe hata vyombo vya makopo vyote pia. 25 Katika siku ile, asema Bwana wa majeshi, ule msumari uliokazwa katika mahali palipo imara utalegea; nao utakatwa na kuanguka chini, na ule mzigo uliokuwa juu yake utakatiliwa mbali; maana Bwana amesema haya.