Un clic sur un verset envoie vers le comparateur de versions.
Lévitique 9.18 Bible en Swahili de l’est
Premiers sacrifices offerts par Aaron et ses fils
1 Basi ilikuwa siku ya nane, Musa akawaita Haruni na wanawe, pamoja na wazee wa Israeli; 2 akamwambia Haruni, Twaa wewe mwana-ng’ombe mume awe sadaka ya dhambi, na kondoo mume wa sadaka ya kuteketezwa, wakamilifu, ukawasongeze mbele ya Bwana. 3 Nawe utawaambia wana wa Israeli, ukisema, Twaeni mbuzi mume awe sadaka ya dhambi; na mwana-ng’ombe, na mwana-kondoo, wote wa mwaka wa kwanza, wakamilifu, kwa sadaka ya kuteketezwa; 4 na ng’ombe mume, na kondoo mume, kwa sadaka za amani, ili kuwachinja mbele za Bwana; na sadaka ya unga uliochanganywa na mafuta; kwa maana, Bwana hivi leo atawatokea. 5 Nao wakayaleta hayo yaliyoagizwa na Musa wakayaweka mbele ya hema ya kukutania; kisha mkutano wote ukakaribia wakasimama mbele za Bwana. 6 Kisha Musa akasema, Neno aliloliagiza Bwana kwamba mlifanye ni hili; na huo utukufu wa Bwana utawatokea. 7 Musa akamwambia Haruni, Ikaribie madhabahu, uitoe sadaka yako ya dhambi, na sadaka yako ya kuteketezwa, ukafanye upatanisho kwa ajili ya nafsi yako, na kwa ajili ya watu; nawe uitoe hiyo dhabihu ya watu, ukafanye upatanisho kwa ajili yao; kama Bwana alivyoagiza. 8 Basi Haruni akakaribia madhabahuni, akamchinja huyo mwana-ng’ombe wa sadaka ya dhambi, aliyekuwa kwa ajili ya nafsi yake. 9 Kisha wana wa Haruni wakamsongezea Haruni ile damu; naye akatia kidole chake katika damu, na kuitia katika pembe za madhabahu, kisha akaimwaga hiyo damu hapo chini ya madhabahu; 10 lakini mafuta, na figo, na kitambi kilichotoka katika ini ya hiyo sadaka ya dhambi, akaviteketeza juu ya madhabahu, kama Bwana alivyomwagiza Musa. 11 Na nyama, na ngozi akazichoma moto nje ya marago. 12 Naye akaichinja sadaka ya kuteketezwa; na wanawe Haruni wakamsongezea ile damu, naye akainyunyiza katika madhabahu pande zote. 13 Nao wakamletea sadaka ya kuteketezwa kipande kwa kipande, na kichwa; naye akaviteketeza juu ya madhabahu. 14 Kisha akaosha matumbo, na miguu na kuiteketeza juu ya hiyo sadaka ya kuteketezwa madhabahuni. 15 Kisha akaisongeza dhabihu ya watu, akamtwaa mbuzi wa sadaka ya dhambi aliyekuwa kwa hao watu, na kumchinja, na kumtoa kwa ajili ya dhambi kama yule wa kwanza. 16 Kisha akaisongeza sadaka ya kuteketezwa, na kuitoa sawasawa na sheria. 17 Kisha akaisongeza sadaka ya unga, na kutwaa konzi humo, na kuiteketeza juu ya madhabahu, pamoja na sadaka ya kuteketezwa ya asubuhi. 18 Huyo ng’ombe mume naye akamchinja, na huyo kondoo mume pia, dhabihu ya sadaka za amani, zilizokuwa kwa ajili ya watu; na wanawe Haruni wakamsongezea ile damu, naye akainyunyiza katika madhabahu pande zote, 19 na mafuta ya ng’ombe; na ya kondoo, mkia wake wa mafuta, na hayo yafunikayo matumbo, na figo zake, na kitambi cha ini; 20 nao wakayaweka hayo mafuta juu ya vidari, naye akayateketeza mafuta juu ya madhabahu; 21 na vile vidari, na mguu wa nyuma wa upande wa kuume, Haruni akavitikisa huku na huku viwe sadaka ya kutikiswa mbele ya Bwana; kama Musa alivyoagiza. 22 Kisha Haruni akainua mikono yake na kuielekeza kwa hao watu, akawabariki; kisha akashuka akisha isongeza sadaka ya dhambi, na sadaka ya kuteketezwa, na sadaka za amani. 23 Kisha Musa na Haruni wakaingia ndani ya hema ya kukutania, kisha wakatoka nje, na kuwabarikia watu; na huo utukufu wa Bwana ukawatokea watu wote. 24 Kisha moto ukatoka hapo mbele za Bwana, na kuiteketeza sadaka ya kuteketezwa, na yale mafuta juu ya madhabahu; watu wote walipouona huo moto wakapiga kelele wakainama kifudifudi.