Un clic sur un verset envoie vers le comparateur de versions.
Matthieu 4.22 Bible en Swahili de l’est
Tentation de Jésus-Christ
Voir Matthieu 4.1 en vidéo
1 Kisha Yesu alipandishwa na Roho nyikani, ili ajaribiwe na Ibilisi. 2 Akafunga siku arobaini mchana na usiku, mwisho akaona njaa. 3 Mjaribu akamjia akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, amuru kwamba mawe haya yawe mikate. 4 Naye akajibu akasema, Imeandikwa, Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu. 5 Kisha Ibilisi akamchukua mpaka mji mtakatifu, akamweka juu ya kinara cha hekalu, 6 akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu jitupe chini; kwa maana imeandikwa, Atakuagizia malaika zake; Na mikononi mwao watakuchukua; Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe. 7 Yesu akamwambia, Tena imeandikwa, Usimjaribu Bwana Mungu wako. 8 Kisha Ibilisi akamchukua mpaka mlima mrefu mno, akamwonyesha milki zote za ulimwengu, na fahari yake, 9 akamwambia, Haya yote nitakupa, ukianguka kunisujudia. 10 Ndipo Yesu alipomwambia, Nenda zako, Shetani; kwa maana imeandikwa, Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake. 11 Kisha Ibilisi akamwacha; na tazama, wakaja malaika wakamtumikia.
Début du ministère de Jésus
12 Basi Yesu aliposikia ya kwamba Yohana amefungwa, alikwenda zake mpaka Galilaya; 13 akatoka Nazareti, akaja akakaa Kapernaumu, mji ulioko pwani, mipakani mwa Zabuloni na Naftali; 14 ili litimie neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, 15 Nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali, Njia ya bahari, ng’ambo ya Yordani, Galilaya ya mataifa, 16 Watu wale waliokaa katika giza Wameona mwanga mkuu, Nao waliokaa katika nchi na uvuli wa mauti Mwanga umewazukia. 17 Tokea wakati huo Yesu alianza kuhubiri, na kusema, Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia. 18 Naye alipokuwa akitembea kando ya bahari ya Galilaya, aliona ndugu wawili, Simoni aitwaye Petro, na Andrea nduguye, wakitupa jarife baharini; kwa maana walikuwa wavuvi. 19 Akawaambia, Nifuateni, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu. 20 Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata. 21 Akaendelea mbele, akaona ndugu wengine wawili, Yakobo wa Zebedayo, na Yohana nduguye, ambao walikuwamo chomboni pamoja na Zebedayo baba yao, wakizitengeneza nyavu zao; akawaita. 22 Mara wakakiacha chombo na baba yao, wakamfuata. 23 Naye alikuwa akizunguka katika Galilaya yote, akifundisha katika masinagogi yao, na kuihubiri Habari Njema ya ufalme, na kuponya ugonjwa na udhaifu wa kila namna katika watu. 24 Na habari zake zikaenea katika Shamu yote; wakamletea wote waliokuwa hawawezi, walioshikwa na maradhi mbalimbali na mateso, wenye pepo, na wenye kifafa, na wenye kupooza; akawaponya. 25 Na makutano mengi wakamfuata, kutoka Galilaya, na Dekapoli, na Yerusalemu, na Uyahudi, na ng’ambo ya Yordani