Un clic sur un verset envoie vers le comparateur de versions.
Job 24.5 Bible en Swahili de l’est
1 Mbona nyakati zisiwekwe na Mwenyezi? Na hao wamjuao mbona hawazioni siku zake? 2 Wako waziondoao alama za mipaka; Huyachukua makundi kwa jeuri na kuyalisha. 3 Humfukuza punda wake asiye baba, Humtwaa rehani ng’ombe wake mwanamke mjane. 4 Humgeuza mhitaji aiache njia; Maskini wa nchi hujificha pamoja. 5 Tazama, kama punda-mwitu jangwani Wao hutoka kwenda kazini mwao, wakitafuta chakula kwa bidii; Jangwa huwapa chakula cha watoto wao. 6 Hukata nafaka zao mashambani; Na kuokota zabibu za waovu. 7 Hujilaza usiku kucha uchi pasipo nguo, Wala hawana cha kujifunika baridi. 8 Hutota kwa manyunyo ya milimani, Na kuambatana na jabali kwa kukosa sitara, 9 Wako wamwondoao matitini kwa nguvu huyo asiye na baba, Na kutwaa rehani kwa maskini; 10 Hata wazunguke uchi pasipo mavazi, Nao wakiwa na njaa huchukua miganda; 11 Hushindika mafuta ndani ya makuta ya watu hao; Wakanyaga mashinikizo, nao wana kiu. 12 Watu huugua toka mji ulio na watu wengi, Na roho yake aliyejeruhiwa hupiga ukelele; Wala Mungu hauangalii upumbavu. 13 Hawa ni katika hao waliouasi mwanga; Hawazijui njia zake, Wala hawakai katika mapito yake. 14 Mwuaji huamka asubuhi kukipambauka, huwaua maskini na wahitaji; Tena wakati wa usiku yu kama mwivi. 15 Tena jicho lake mzinifu hungojea wakati wa giza-giza, Akisema, Hapana jicho litakaloniona; Naye huuficha uso wake. 16 Wao hutoboa nyumba gizani; Hujifungia ndani wakati wa mchana; Hawaujui mwanga. 17 Kwani asubuhi kwao wote ni kama giza tupu; Kwani wao wavijua vitisho vya hiyo giza tupu. 18 Mwasema, Yeye ni mwepesi juu ya uso wa gharika; Sehemu yao inalaaniwa duniani; Hageuki kwenda njia ya mizabibuni. 19 Chaka na hari hukausha maji ya theluji; Kuzimu nako hao ambao wamefanya dhambi. 20 Tumbo lililomzaa litamsahau; buu litamla na kuona tamu; Hatakumbukwa tena; Na udhalimu utavunjwa kama mti. 21 Naam, yeye huwala walio tasa wasiozaa; Wala hamtendei mema mwanamke mjane. 22 Lakini Mungu huwadumisha wenye uwezo kwa nguvu zake; Huinuka, wasiokuwa na tumaini la kuishi. 23 Huwapa kuwa na salama, nao wapumzika kwayo; Na macho yake ya juu ya njia zao. 24 Wao wametukuzwa; lakini kitambo kidogo hutoweka; Naam, hushushwa, na kuondolewa njiani kama wengine wote, Nao hukatwa kama vile masuke ya ngano. 25 Na kama sivyo sasa, ni nani atakayenihukumu kuwa ni mwongo, Na kuyafanya maneno yangu kuwa si kitu?