Fermer le panneau de recherche

Appuyez sur Entrée pour rechercher ou ESC pour annuler.

Job 39
Bible en Swahili de l’est


1 Je! Wajua majira ya kuzaa kwao mbuzi-mwitu walio majabalini? Au waweza kusema majira ya kuzaa kulungu? 2 Je! Waweza kuhesabu miezi yao watakayoitimiza? Au je! Wajua majira ya kuzaa kwao? 3 Wao hujiinamisha, kuzaa watoto wao, Watupa taabu zao. 4 Watoto wao wa katika hali nzuri, hukua katika bara wazi; Huenda zao, wala hawarudi tena. 5 Ni nani aliyempeleka punda-milia aende huru? Au je! Ni nani aliyemfungulia vifungo punda-mwitu? 6 Ambaye nimeifanya nyika kuwa nyumba yake, Na nchi ya chumvi kuwa makao yake. 7 Yeye hudharau mshindo wa mji, Wala hasikii kelele zake msimamizi. 8 Upana wa milima ni malisho yake, Hutafuta-tafuta kila kitu kilicho kibichi. 9 Je! Nyati atakubali kukutumikia? Au atakaa katika zizi lako? 10 Je! Waweza kumfunga nyati kwa kamba matutani? Au, yeye atayalima mabonde nyuma yako? 11 Je! Utamtumaini kwa sababu ana nguvu nyingi? Au, utamwachia yeye kazi yako? 12 Je! Utamtumaini kwamba ataileta mbegu yako nyumbani. Na kukusanya nafaka ya kiwanja chako cha kupuria? 13 Bawa la mbuni hufurahi; Lakini mabawa yake na manyoya yake, je! Yana huruma? 14 Kwani yeye huyaacha mayai yake juu ya nchi, Na kuyatia moto mchangani, 15 Na kusahau kwamba yumkini mguu kuyavunja, Au mnyama wa mwitu kuyakanyaga. 16 yeye huyafanyia ukali makinda yake, kana kwamba si yake; Ijapokuwa taabu yake ni ya bure, hana hofu; 17 Kwa sababu Mungu amemnyima akili, Wala hakumpa fahamu. 18 Wakati anapojiinua juu aende, Humdharau farasi na mwenye kumpanda. 19 Je! Wewe ulimpa farasi uwezo wake? Au, ni wewe uliyemvika shingo yake manyoya yatetemayo? 20 Ndiwe uliyemfanya aruke kama nzige? Fahari ya mlio wake hutisha. 21 Hupara-para bondeni, na kuzifurahia nguvu zake; Hutoka kwenda kukutana na wenye silaha. 22 Yeye hufanyia kicho dhihaka, wala hashangai; Wala hageuki kurudi nyuma mbele ya upanga. 23 Podo humpigia makelele, Mkuki ung’aao na fumo. 24 Huimeza nchi kwa ukali wake na ghadhabu; Wala hasimami kwa sauti ya baragumu. 25 Kila ipigwapo baragumu yeye husema, Aha! Naye husikia harufu ya vita toka mbali, Mshindo wa maakida, na makelele. 26 Je! Mwewe huruka juu kwa akili zako, Na kuyanyosha mabawa yake kwenda kusini? 27 Je! Tai hupaa juu kwa amri yako, Na kufanya kioto chake mahali pa juu? 28 Hukaa jabalini, ndiko kwenye malazi yake, Juu ya genge la jabali, na ngomeni. 29 Toka huko yeye huchungulia mawindo; Macho yake huyaangalia toka mbali. 30 Makinda yake nayo hufyonza damu; Na kwenye maiti ndiko aliko.

Cette Bible est dans le domaine public.