Fermer le panneau de recherche

Appuyez sur Entrée pour rechercher ou ESC pour annuler.

Proverbes 28
Bible en Swahili de l’est


1 Waovu hukimbia wasipofuatiwa na mtu; Bali wenye haki ni wajasiri kama simba. 2 Kwa sababu ya maasi ya nchi wakuu wake huwa wengi; Bali kwa wenye ufahamu na maarifa hali ya nchi hudumishwa 3 Mtu mhitaji awaoneaye maskini, Ni kama mvua ya dhoruba isiyosaza chakula. 4 Wao waiachao sheria huwasifu waovu; Bali wao waishikao hushindana nao. 5 Watu wabaya hawaelewi na hukumu; Bali wamtafutao Bwana huelewa na yote. 6 Afadhali maskini aendaye katika unyofu wake, Kuliko mpotofu wa njia angawa ni tajiri. 7 Yeye aishikaye sheria ni mwana mwenye hekima; Bali aliye rafiki wa walafi humwaibisha babaye. 8 Yeye azidishaye mali yake kwa riba na faida, Humkusanyia mtu awahurumiaye maskini. 9 Yeye aligeuzaye sikio lake asiisikie sheria, Hata sala yake ni chukizo. 10 Kila mtu awapotezaye wenye haki katika njia mbaya, Ataanguka katika rima lake mwenyewe; Bali wakamilifu watarithi mema. 11 Mtu tajiri ana hekima machoni pake mwenyewe; Bali maskini mwenye ufahamu humchunguza sana. 12 Wenye haki washindapo, uko utukufu mwingi; Bali waovu waondokapo, watu hujificha. 13 Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema. 14 Mwanadamu mwenye kicho yu heri sikuzote; Bali mshupavu wa moyo ataangukia madhara. 15 Kama simba angurumaye, na dubu mwenye njaa; Ndivyo alivyo mtu mbaya awatawalaye maskini. 16 Mkuu aliyepungukiwa na akili huwaonea watu sana; Bali achukiaye kutamani ataongeza siku zake. 17 Aliyelemewa na damu ya mtu Atalikimbilia shimo; wala mtu asimzuie. 18 Aendaye kwa unyofu ataokolewa; Bali mkaidi wa njia zake ataanguka mara. 19 Alimaye shamba lake atakuwa na chakula tele; Bali afuataye mambo ya upuzi atapata umaskini wa kumtosha. 20 Mtu mwaminifu atakuwa na baraka tele; Lakini afanyaye haraka kuwa tajiri hakosi ataadhibiwa. 21 Kupendelea watu si kwema; Wala mtu kuasi kwa ajili ya kipande cha mkate. 22 Mwenye husuda afanya haraka kuwa tajiri; Wala haufikiri uhitaji utakaomjilia. 23 Amkemeaye mwenzake hatimaye atapata kibali; Zaidi ya mtu ajipendekezaye kwa ulimi wake. 24 Aibaye mali ya babaye au mamaye, na kusema, Si kosa; Mwana huyo ni rafiki wa mtu mharibifu. 25 Mwenye nafsi ya kutamani huchochea fitina; Bali amtumainiye Bwana atawandishwa. 26 Mwenye kujitumainia moyo wake ni mjinga; Bali yeye aendaye kwa busara ataokolewa. 27 Mwenye kuwagawia maskini hatahitaji kitu; Bali afichaye macho yake atakuwa na laana nyingi. 28 Wasio haki wainukapo, wanadamu hujificha; Bali waangamiapo, wenye haki huongezeka.

Cette Bible est dans le domaine public.