Fermer le panneau de recherche

Appuyez sur Entrée pour rechercher ou ESC pour annuler.

Psaumes 104
Bible en Swahili de l’est


1 Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana. Wewe, Bwana, Mungu wangu, Umejifanya mkuu sana; Umejivika heshima na adhama. 2 Umejivika nuru kama vazi; Umezitandika mbingu kama pazia; 3 Na kuziweka nguzo za orofa zake majini. Huyafanya mawingu kuwa gari lake, Na kwenda juu ya mabawa ya upepo, 4 Huwafanya malaika zake kuwa pepo, Na watumishi wake kuwa moto wa miali. 5 Uliiweka nchi juu ya misingi yake, Isitikisike milele. 6 Uliifunika kwa vilindi kama kwa vazi, Maji yalikuwa yakisimama juu ya milima. 7 Kwa kukemea kwako yakakimbia, Kwa sauti ya radi yako yakaenda zake kasi, 8 Yakapanda milima, yakatelemka mabondeni, Mpaka mahali ulipoyatengenezea. 9 Umeweka mpaka yasiupite, Wala yasirudi kuifunikiza nchi. 10 Hupeleka chemchemi katika mabonde; Zapita kati ya milima; 11 Zamnywesha kila mnyama wa kondeni; Punda mwitu huzima kiu yao. 12 Kandokando hukaa ndege wa angani; Kati ya matawi hutoa sauti zao. 13 Huinywesha milima toka orofa zake; Nchi imeshiba mazao ya kazi zako. 14 Huyameesha majani kwa makundi, Na maboga kwa matumizi ya mwanadamu; Ili atoe chakula katika nchi, 15 Na divai imfurahishe mtu moyo wake. Aung’aze uso wake kwa mafuta, Na mkate umburudishe mtu moyo wake. 16 Miti ya Bwana nayo imeshiba, Mierezi ya Lebanoni aliyoipanda. 17 Ndimo ndege wafanyamo vitundu vyao, Na korongo, misunobari ni nyumba yake. 18 Milima mirefu ndiko waliko mbuzi wa mwitu, Na magenge ni kimbilio la wibari. 19 Aliufanya mwezi kwa ajili ya nyakati, Jua latambua kuchwa kwake. 20 Wewe hufanya giza, kukawa usiku, Ndipo atambaapo kila mnyama wa mwitu. 21 Wana-simba hunguruma wakitaka mawindo, Ili kutafuta chakula chao kwa Mungu. 22 Jua lachomoza, wanakwenda zao, Na kujilaza mapangoni mwao. 23 Mwanadamu atoka kwenda zake kazini, Na kwenye utumishi wake mpaka jioni. 24 Ee Bwana, jinsi yalivyo mengi matendo yako! Kwa hekima umevifanya vyote pia. Dunia imejaa mali zako. 25 Bahari iko kule, kubwa na upana, Ndimo mlimo viendavyo visivyohesabika, Viumbe hai vidogo kwa vikubwa. 26 Ndimo zipitamo merikebu, Ndimo alimo lewiathani uliyemwumba acheze humo. 27 Hao wote wanakungoja Wewe, Uwape chakula chao kwa wakati wake. 28 Wewe huwapa, Wao wanakiokota; Wewe waukunjua mkono wako, Wao wanashiba mema; 29 Wewe wauficha uso wako, Wao wanafadhaika; Waiondoa pumzi yao, wanakufa, Na kuyarudia mavumbi yao, 30 Waipeleka roho yako, wanaumbwa, Nawe waufanya upya uso wa nchi. 31 Utukufu wa Bwana na udumu milele; Bwana na ayafurahie matendo yake. 32 Aitazama nchi, inatetemeka; Aigusa milima, inatoka moshi. 33 Nitamwimbia Bwana maadamu ninaishi; Nitamshangilia Mungu wangu nikiwa hai; 34 Kutafakari kwangu na kuwe kutamu kwake; Mimi nitamfurahia Bwana. 35 Wenye dhambi waangamizwe katika nchi, Watendao ubaya wasiwepo tena. Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana.

Cette Bible est dans le domaine public.