Un clic sur un verset envoie vers le comparateur de versions.
Romains 1.5 Bible en Swahili de l’est
Une justice obtenue par la foi
Salutation et louange
1 Paulo, mtumwa wa Kristo Yesu, aliyeitwa kuwa mtume, na kutengwa aihubiri Injili ya Mungu; 2 ambayo Mungu amekwisha kuiahidi kwa kinywa cha manabii wake katika maandiko matakatifu; 3 yaani, habari za Mwanawe, aliyezaliwa katika ukoo wa Daudi kwa jinsi ya mwili, 4 na kudhihirishwa kwa uweza kuwa Mwana wa Mungu, kwa jinsi ya roho ya utakatifu, kwa ufufuo wa wafu, Yesu Kristo Bwana wetu; 5 ambaye katika yeye tulipokea neema na utume ili mataifa yote wapate kujitiisha kwa imani, kwa ajili ya jina lake; 6 ambao katika hao ninyi mmekuwa wateule wa Yesu Kristo; 7 kwa wote walioko Rumi, wapendwao na Mungu, walioitwa kuwa watakatifu. Neema na iwe kwenu na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu, na kwa Bwana Yesu Kristo. 8 Kwanza namshukuru Mungu wangu katika Yesu Kristo kwa ajili yenu nyote, kwa kuwa imani yenu inahubiriwa katika dunia nzima. 9 Kwa maana Mungu, nimwabuduye kwa roho yangu katika Injili ya Mwana wake, ni shahidi wangu jinsi niwatajavyo pasipo kukoma, 10 siku zote katika sala zangu, nikiomba nije kwenu hivi karibu, Mungu akipenda kuifanikisha safari yangu. 11 Kwa maana ninatamani sana kuwaona, nipate kuwapa karama ya rohoni, ili mfanywe imara; 12 yaani, tufarijiane mimi na ninyi, kila mtu kwa imani ya mwenzake, yenu na yangu. 13 Lakini, ndugu zangu, sipendi msiwe na habari, ya kuwa mara nyingi nalikusudia kuja kwenu, nikazuiliwa hata sasa, ili nipate kuwa na matunda kwenu ninyi pia kama nilivyo nayo katika Mataifa wengine. 14 Nawiwa na Wayunani na wasio Wayunani, nawiwa na wenye hekima na wasio na hekima. 15 Kwa hiyo, kwa upande wangu, mimi ni tayari kuihubiri Injili hata na kwenu ninyi mnaokaa Rumi. 16 Kwa maana siionei haya Injili; kwa sababu ni uweza wa Mungu uuletao wokovu, kwa kila aaminiye, kwa Myahudi kwanza, na kwa Myunani pia. 17 Kwa maana haki ya Mungu inadhihirishwa ndani yake, toka imani hata imani; kama ilivyoandikwa, Mwenye haki ataishi kwa imani.
Culpabilité des non-Juifs
18 Kwa maana ghadhabu ya Mungu imedhihirishwa kutoka mbinguni juu ya uasi wote na uovu wa wanadamu waipingao kweli kwa uovu. 19 Kwa kuwa mambo ya Mungu yanayojulikana yamekuwa dhahiri ndani yao, kwa maana Mungu aliwadhihirishia. 20 Kwa sababu mambo yake yasiyoonekana tangu kuumbwa ulimwengu yanaonekana, na kufahamika kwa kazi zake; yaani, uweza wake wa milele na Uungu wake; hata wasiwe na udhuru; 21 kwa sababu, walipomjua Mungu hawakumtukuza kama ndiye Mungu wala kumshukuru; bali walipotea katika uzushi wao, na mioyo yao yenye ujinga ikatiwa giza. 22 Wakijinena kuwa wenye hekima walipumbazika; 23 wakaubadili utukufu wa Mungu asiye na uharibifu kwa mfano wa sura ya binadamu aliye na uharibifu, na ya ndege, na ya wanyama, na ya vitambaavyo. 24 Kwa ajili ya hayo Mungu aliwaacha katika tamaa za mioyo yao, waufuate uchafu, hata wakavunjiana heshima miili yao. 25 Kwa maana waliibadili kweli ya Mungu kuwa uongo, wakakisujudia kiumbe na kukiabudu badala ya Muumba anayehimidiwa milele. Amina. 26 Hivyo Mungu aliwaacha wafuate tamaa zao za aibu, hata wanawake wakabadili matumizi ya asili kwa matumizi yasiyo ya asili; 27 wanaume nao vivyo hivyo waliyaacha matumizi ya mke, ya asili, wakawakiana tamaa, wanaume wakiyatenda yasiyopasa, wakapata nafsini mwao malipo ya upotevu wao yaliyo haki yao. 28 Na kama walivyokataa kuwa na Mungu katika fahamu zao, Mungu aliwaacha wafuate akili zao zisizofaa, wayafanye yasiyowapasa. 29 Wamejawa na udhalimu wa kila namna, uovu na tamaa na ubaya; wamejawa na husuda, na uuaji, na fitina, na hadaa; watu wa nia mbaya, wenye kusengenya, 30 wenye kusingizia, wenye kumchukia Mungu, wenye jeuri, wenye kutakabari, wenye majivuno, wenye kutunga mabaya, wasiowatii wazazi wao, 31 wasio na ufahamu, wenye kuvunja maagano, wasiopenda jamaa zao, wasio na rehema; 32 ambao wakijua sana hukumu ya haki ya Mungu, ya kwamba wayatendao hayo wamestahili mauti, wanatenda hayo, wala si hivyo tu, bali wanakubaliana nao wayatendao.